Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, mashindano hayo yaliyoandaliwa na idara ya kimataifa ya Kiislamu kwa kushirikiana na taasisi ya kimataifa ya kuhifadhi Qur'ani, yamefanyika katika chuo cha udaktari jijini Bujumbura, mji mkuu wa Burundi. Washiriki 85 miongoni mwa wasichana na wavulana walichuana katika nafasi tano za kuhifadhi Qur'ani, kuanzia juzu tatu, juzu tano, juzu saba, juzu 15 na Qur'ani nzima sanjari na kusimamiwa na waamuzi wanne katika nyanja tofauti. Fadhil Juma, mjumbe wa baraza kuu nchini Burundi, Abdul-Wahhab Yahya al-Sirar, mjumbe wa jumuiya ya kimataifa ya kuhifadhi Qur'ani, viongozi wa taasisi kadhaa za Kiislamu, wakuu na walimu wa madrasa, ni miongoni mwa shakhsia waliohudhuria mashindano hayo ya Qur'ani Tukufu.