IQNA

Pep Guardiola ataka haki, aangazia maumivu ya Wapalestina

15:53 - January 30, 2026
Habari ID: 3481871
IQNA – Pep Guardiola kocha wa timu ya Ligi Kuu ya Soka Uingereza (EPL), Manchester City, ameeleza hadharani uungaji mkono wake kwa wananchi wa Palestina, akielekeza macho ya ulimwengu kwenye janga kubwa la kibinadamu linaloikumba Gaza, wakati wa tukio la hadhara lililofanyika hivi karibuni.

Guardiola alieleza msimamo wake wazi siku ya Alhamisi katika kongamano lililoandaliwa sambamba na kampeni ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Palestina mjini Barcelona. Akiwa amevaa kitambaa cha Kipalestina ambacho ni maarufu kama keffiyeh, alianza hotuba yake kwa lugha ya Kiarabu akisema: “As-salāmu ‘alaykum (Amani iwe juu yenu).”

Kauli zake zilithibitisha tena mshikamano wake na Wapalestina, zikatoa mwanga juu ya kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, na kufufua mjadala kuhusu wajibu wa jumuiya ya kimataifa katika kuwalinda raia wasio na hatia.

Katika hotuba yake, Guardiola aliashiria picha za watoto wa Kipalestina waliopoteza wazazi wao chini ya vifusi vya nyumba zilizobomolewa kwa mabomu. Alisema: “Nilipoona mtoto akimlilia mama yake, aliyefukiwa chini ya vifusi, nilihisi kuwa tumewaacha peke yao, tumewatelekeza, tumewasahau.”

Aliitaja mateso ya watoto hao kuwa ni kilio cha moja kwa moja kwa ulimwengu mzima. “Daima namwona mtoto huyu kana kwamba anasema: Mko wapi? Njooni mtusaidie. Na hadi sasa, hatujafanya hivyo.”

Guardiola alisisitiza kuwa ukimya wa kimataifa unaongeza madhara. “Kile ambacho mabomu husababisha, na wanachotaka kusababisha, ni ukimya. Wanataka tutazame pembeni. Hilo ndilo lengo lao pekee.”

Pia alitoa lawama kali kwa viongozi wa kisiasa, akiwataja kuwa ni “mamlaka ya woga.” “Wanawatuma vijana wasio na hatia kuwaua watu wasio na hatia,” alisema, “wakati wao wanabaki majumbani mwao, wakiwa na joto wakati wa baridi na kiyoyozi wakati wa joto.”

Alisisitiza kuwa kuchukua hatua huanza kwa kukataa kunyamaza. “Ni lazima tupige hatua mbele. Kuwepo tu tayari kuna maana kubwa, maana kubwa sana.”

Habari inayohusiana:

Guardiola alihitimisha kwa ujumbe wazi wa mshikamano: “Tunasimama mbele ya dunia kuonyesha kuwa tuko upande wa walio dhaifu zaidi. Katika hali hii, hao ni Wapalestina, na kila kadhia ya haki.”

Msimamo wake unaangazia msimamo wa kimaadili wa mmoja wa watu mashuhuri zaidi katika ulimwengu wa michezo, huku pia ukiongeza shinikizo kwa serikali na taasisi za kimataifa kuchukua hatua, akionya kuwa ukimya au kutojali ni sawa na kusaliti haki za msingi za binadamu.

3496236

captcha