IQNA

Zawadi Tukufu: Mayatima wa Jordan watekeleza Umrah baada ya kung’ara katika kuhifadhi Qur’ani Tukufu

15:16 - January 30, 2026
Habari ID: 3481869
IQNA – Yatima arobaini na wanane nchini Jordan wamepata thawabu tukufu ya safari ya Umrah iliyogharamiwa kikamilifu, baada ya kung’ara katika mashindano ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu.

Shirika la Sharjah Charity International limeandaa safari hiyo ya Umrah kwa mayatima 48 wanaodhaminiwa nchini Jordan, baada ya kuibuka washindi katika Mashindano ya Kuhifadhi Qur’ani Tukufu yaliyoandaliwa hivi karibuni kama sehemu ya programu zake endelevu kwa wanufaika.

Kikundi hicho, kikifuatana na wasimamizi, kilisafiri kuelekea maeneo matukufu kutekeleza ibada ya Umrah, ikiwa ni heshima na kutambua juhudi zao na mafanikio yao katika kuhifadhi Qur’ani Tukufu.

Mohammed Abdulrahman Al Ali, Mkurugenzi wa Idara ya Udhamini na Malezi ya Yatima, amesema kuwa wanufaika hao waliondoka Jordan wakiwa na furaha kubwa, hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao walikuwa wakitekeleza Umrah kwa mara ya kwanza maishani mwao. Safari hiyo iliwezekana kupitia msaada wa wahisani wanaochangia kampeni na miradi ya kheri ya shirika hilo.

Ameongeza kuwa mpango huu ni ishara ya kuthamini juhudi za washindi, sambamba na kuhamasisha vijana kusoma, kuhifadhi na kutafakari Qur’ani Tukufu, jambo linalosaidia kupandikiza maadili na misingi yake mema ndani ya jamii.

Al Ali pia alieleza kuwa mpango huo ulipokelewa kwa mwitikio chanya mkubwa tangu uzinduzi wa mashindano, kutangazwa kwa washindi, hadi kuandaliwa kwa safari ya Umrah, iliyowawezesha washiriki kuitembelea Msikiti Mtukufu wa Makka (Al-Masjid al-Haram) na kutekeleza ibada takatifu.

Habari inayohusiana:

Sharjah Charity International ilisimamia kikamilifu maandalizi yote ya safari, yakiwemo utoaji wa visa, uhifadhi wa tiketi za ndege, malazi Makka na Madina, pamoja na usafiri wa ndani, ili kuhakikisha safari ilikuwa salama, nyepesi na yenye faraja. Wasimamizi maalum waliandamana na kikundi hicho kuwaongoza mahujaji na kuhakikisha utekelezaji sahihi wa ibada za Umrah.

Mwisho, Al Ali alitoa shukrani zake za dhati kwa wahisani wote kwa msaada wao endelevu kwa programu za shirika hilo, na pia akatoa pongezi kwa Ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini Jordan kwa mchango wake muhimu katika kusaidia utekelezaji wa miradi ya kibinadamu na misaada ya kheri.

3496235

Habari zinazohusiana
captcha