IQNA

Risala ya Tanzia kufuatia kufariki dunia Ayatullah Bahjat

10:18 - May 19, 2009
Habari ID: 1779967
Kufuatia kufariki dunia Ayatullah Alhaj Sheikh Muhammad Taqi Bahjat tarehe 17 Mei katika mji wa Qom, Iran, akiwa na umri wa miaka 96, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ametuma risala ifuatayo.
Bismillahir Rahmanir Rahim
Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea. (al Baqarah 2:156).
Nimeipokea kwa majonzi na masikitiko makubwa habari ya kufariki dunia Aalim, mwanachuoni, arif na mcha Mungu mkubwa, Ayatullah Alhaj Sheikh Muhammad Taqi Bahjat (Mwenyezi Mungu aitukuze nafsi yake safi).
Msiba huu kwangu mimi na kwa wapenzi wote wa Bwana huyu mkubwa ni msiba mzito ulioacha pengo lisilozibika.
Anapofariki dunia mwanachuoni hubakia pengo lisilozibika katika Uislamu hadi siku ya kiyama.
Mtukufu huyo alikuwa miongoni mwa marajii wakubwa katika zama hizi, alikuwa ni mwalimu mkubwa wa akhlaki na irfan na alikuwa ni chemchem ya mawimbi ya umaanawi usio na kikomo. Moyo wa mcha Mungu huyo ulikuwa mnyofu na uliojaa nuru, alikuwa ni kioo kilichong'arishwa na ilhamu ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu na alikuwa na maneno ya kuvutia na miongozo ya kifikra na kivitendo kwa wote wanaotafuta njia nyoofu.
Ninatoa mkono wa pole kwa udhati wa moyo wangu na mkono wangu huo wa pole umfikie Imam wa Zama (roho zetu ziwe fidia kwake), na pia uwafikie maulamaa, wanavyuoni, marajii, wanafunzi wake, wafuasi wake na hasa familia ya mwanachuoni huyo mkubwa. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atuondolee majonzi na airehemu na kuighufiria roho toharifu ya mwanachuoni huyu.
Wassalaamu Alayhi Warahmatullah.
Sayyid Ali Khamenei.
27 Ordibehesht 1388.
22 Mfunguo Nane 1480.
17 Mei 2009.

406830
captcha