
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Idd al‑Adhha itaadhimishwa siku ya Jumatano, Mei 27, kufuatia kuthibitishwa kuonekana kwa hilali ya Dhul‑Hijja jioni ya Jumapili.
Kuonekana kwa hilali hiyo huashiria kuanza kwa mwezi ambao ndani yake hufanyika ibada tukufu ya Hija.
Kilele cha ibada ya hija, yaani Siku ya Arafah, kitakuwa Jumanne, Mei 26.
Nchini Iran pia mwezi umeonekana na hivyo sawa na Saudi Arabia, leo 18 Mei ni siku ya kwanza ya Dhul Hija.
Hija ni nguzo ya tano ya Uislamu, na kila Muislamu anatakiwa kuitekeleza angalau mara moja maishani mwake iwapo ana uwezo wa kiafya na kifedha.
Idd al‑Adhha ni miongoni mwa sikukuu kubwa zaidi kwa Waislamu duniani kote, na huadhimishwa kwa muda wa siku moja hadi nne, kulingana na mila na utaratibu wa nchi mbalimbali.
Katika siku ya Idd, mahujaji walioko katika ibada ya Hija hutekeleza ibada ya kuchinja mnyama wa dhabihu. Baada ya hapo, mambo mengi yaliyokuwa haramu wakati wa Ihramuhuruhusiwa tena kwa mahujaji.
Idd al‑Adhha pia ni ukumbusho wa mtihani wa Mwenyezi Mungu kwa Nabii Ibrahim (AS) na mwanawe Ismail (AS) ambao waliupokea kwa utiifu mkubwa na wakafaulu.
Kwa mujibu wa Hadithi za Kiislamu, Nabii Ibrahim alipata mwana katika uzee wake na akamwita Ismail, ambaye alimpenda sana. Ismail alipofikia umri wa ujana, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Ibrahim amchinjie mwanawe huyo kwa kisu.
Ismail alipojulishwa amri hiyo ya Mwenyezi Mungu, alikubali kwa moyo wa utiifu kujitoa katika njia ya Mola wake. Hata hivyo, Nabii Ibrahim alipoweka kisu shingoni mwa mwanawe, Mwenyezi Mungu akamletea kondoo dume, naye akachinjwa badala ya Ismail.
Kisa hiki kimetajwa katika Aya ya 103–105 ya Surah As‑Saffat katika Qur’ani Tukufu:
“Waliponyenyekea wote wawili (kwa amri ya Mwenyezi Mungu), na Ibrahim akamlaza mwanawe kwa upande wa uso wake (kwa ajili ya kuchinja), Tulimwita: ‘Ewe Ibrahim! Hakika umetimiza uliyoamrishwa katika ndoto yako.’ Hivyo ndivyo Tunavyowalipa wanaofanya wema.”
3497500