IQNA

Uchunguzi baada ya watu 5 kuuawa katika hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti Marekani

10:26 - May 19, 2026
Habari ID: 3482256
IQNA – Watu watatu waliokuwa ndani ya Msikiti wa Kituo cha Kiislamu cha San Diego nchini Marekani wamepoteza maisha kufuatia hujuma ya kigaidi Jumatatu. Polisi wamethibitisha kuwa washambuliaji wawili, ambao ni vijana, pia wamefariki dunia, na kufanya jumla ya watu watano kupoteza maisha katika tukio ambalo maafisa wanaliita shambulizi linaloweza kuwa limechochewa na chuki dhidi ya Uislamu.

Tukio hilo la kigaidi lilitokea muda mfupi kabla ya adhana ya adhuhuri katika msikiti huo ulioko mtaa wa Clairemont, jambo lililosababisha msako mkubwa wa vyombo vya usalama na kuzua hofu kubwa miongoni mwa jamii za Waislamu kote California.

Kamishna wa Polisi wa San Diego, Scott Wahl, amesema maafisa walifika eneo la tukio ndani ya dakika nne baada ya kupata ripoti za ufyatuaji risasi. Polisi walikuta watu watatu wazima wakiwa wamepigwa risasi nje ya msikiti huo, akiwemo mlinzi ambaye maafisa wamemsifu kwa juhudi zake za kusaidia kuzuia vifo zaidi.

“Mlinzi huyo alikuwa na jukumu kubwa la kuzuia janga hili kuwa kubwa zaidi,” Wahl aliwaambia wanahabari katika mkutano.

Wakati maafisa wakifanya msako katika msikiti na maeneo ya jirani, ripoti nyingine za milio ya risasi zilisikika mita chache kutoka hapo. Baadaye, mamlaka ziliwakuta washukiwa hao wawili, wenye umri wa miaka 17 na 19, wakiwa wamefariki ndani ya gari kutokana na majeraha ya risasi wanayodhaniwa kujipiga wenyewe.

Wapelelezi wameanza kuchunguza iwapo itikadi kali za chuki dhidi ya Uislamu zilichangia shambulizi hilo la kigaidi. Kwa mujibu wa gazeti la Los Angeles Times, wapelelezi waligundua maandishi ya chuki dhidi ya Uislamu, nyenzo za kueneza chuki, na barua ya kujiua inayozungumzia “kiburi cha rangi” (racial pride) ndani ya gari la washukiwa. Mamlaka zinaamini kuwa angalau moja ya silaha zilizotumika inaweza kuwa ilichukuliwa kutoka nyumbani kwa mzazi wa mmoja wa washukiwa.

Ofisi ya Upelelezi ya Shirikisho (FBI) inasaidiana na polisi wa eneo hilo katika uchunguzi, ambao mamlaka zimesema unashughulikiwa kama uchunguzi wa uhalifu wa chuki (hate crime).

Kituo cha Kiislamu cha San Diego, ambacho ni moja ya misikiti mikubwa zaidi katika eneo hilo, kinaendesha pia shule ya Kiislamu iliyoidhinishwa. Polisi waliwahamisha wanafunzi na wafanyakazi wakati wa tukio hilo, na viongozi wa jamii walithibitisha baadaye kuwa hakuna watoto waliojeruhiwa.

“Hili ni tukio la kusikitisha sana,” alisema Deana Helmy, Mwenyekiti wa Baraza la Shura la Kiislamu la California Kusini. “Hii ni nyumba ya ibada. Kuna shule yenye watoto ambao wako hapo kwa ajili ya kupata elimu.”

Gunfire erupted Monday, May 18, 2026, at the Islamic Center of San Diego, leaving three worshippers and two teenage suspects dead.

Taha Hassane, Imamu wa msikiti huo, alisema shambulizi hilo limeitikisa jamii ya Waislamu wa eneo hilo.

“Hatujawahi kushuhudia msiba kama huu hapo awali,” alisema Hassane. “Ni jambo la kusikitisha na lisilokubalika kushambulia nyumba ya ibada.”

Shambulizi hili la kigaidi dhidi ya Waislamu limetokea mwanzoni mwa Dhul-Hijjah, mojawapo ya miezi mitukufu katika kalenda ya Kiislamu, ambapo Waislamu duniani kote wameanza maandalizi ya Ibada ya Hija na sikukuu ya Eid al-Adha.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu, ikiwemo tawi la California la Baraza la Mahusiano ya Kiislamu-Marekani (CAIR), yamesema yanafanya kazi na misikiti yote ya jimbo hilo ili kupitia upya hatua za usalama kufuatia hujuma hiyo ya kigaidi.

Gavana wa California, Gavin Newsom, na Meya wa San Diego, Todd Gloria, wamesema wamepokea taarifa za tukio hilo na kuwashukuru wahudumu wa dharura kwa juhudi zao. Mamlaka zimesema uchunguzi unaendelea ili kubaini kikamilifu mazingira na nia iliyopo nyuma ya shambulizi hilo.

3497513

Habari zinazohusiana
Kishikizo: marekani msikiti mauaji
captcha