IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Hapana shaka kwamba Palestina itarejea katika mikono ya Uislamu

2:45 - June 05, 2011
Habari ID: 2133168
Katika shughuli ya kumbukumbu ya mwaka wa 22 tangu Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu afariki dunia, hii leo wananchi wa Iran ya Kiislamu wameifanya haram ya shakhsia huyo kuwa medani ya kudhihirisha uaminifu wao mkubwa kwa njia na fikra za kiongozi huyo. Maelfu ya wananchi hao wamedhihirisha hisia zao za upendo na mahaba kwa hayati Imam Khomeini na kutangaza tena baia’ na utiifu wao kwa khalifa wa kiongozi wa baada yake, Ayatullah Ali Khamenei.
Mkusanyiko huo mkubwa wa watu wa matabaka mbalimbali ya wananchi kutoka maeneo tofauti ya Iran umehutubiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ambaye amebainisha sifa za mwamko wa sasa wa mataifa ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, mwamko ambao umetimiza utabiri wa hayati Imam Khomeini, na kuongeza kuwa maana halisi ya upendo wa taifa la Iran na kumuenzi Imam ni kukubali na kushikamana na fikra na njia yake. Amesema masuala ya kiroho, mantiki na uadilifu ndio msingi wa mfumo wa kifikra, wenye mlingano na wenye pande kadhaa wa hayati Imam Khomeini na kusisitiza kwamba taifa la Iran litapata heshima, maendeleo na mafanikio kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita kwa baraka za kushikamana na urithi wa thamani uliobakishwa na Imam Ruhullah Khomeini.
Ayatullah Khamenei amesema siku ya tarehe 14 Khordad (Juni 4) ya kila mwaka huwa fursa ya taifa la Iran kumkumbuka Imam Khomeini. Ameashiria kukutana siku hiyo mwaka huu na mwanzo wa mwezi mtukufu wa Rajab na akasema kuwa shughuli ya kukumbuka siku ya kufariki dunia Imam mwaka huu pia imekutana na hamasa ya mwamko wa Kiislamu wa mataifa ya Mashariki na Kati na kaskazini mwa Afrika na kutimiza utabiri wa shakhsia huyo mkubwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mfumo wa kifikra wa Imam Khomeini ni hazina yenye thamani kubwa kwa taifa la Iran na kuongeza kuwa wananchi wa Iran wameweza kuvuka kwa mafanikio kipindi kigumu cha miaka 32 iliyopita kwa kushikamana na utajiri huo mkubwa na hali itaendelea kuwa hivyo katika siku za usoni.
Ameashiria wimbi kubwa la hisia za upendo na mahaba ya taifa la Iran kwa Imam Ruhullah Khomeini na akasema, mahaba na upendo wa wananchi wa Iran kwa Imam hauishii katika hisia hizo za kiroho, bali maana ya hisia hizo ni kukubali na kushikamana barabara na mfumo wake kama njia na sera ya wazi na harakati ya taifa zima.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mfumo wa Imam Khomeini kuwa ndiyo dira na mwongozo wa kinadharia na kimatendo wa wananchi na viongozi. Amesema kuwa mfumo wa Imam ni kifurushi kamili na chenye pande mbalimbali ambazo zinapaswa kutazamwa na kutekelezwa kwa pamoja ili kuepuka makosa na kupotoka njia ya Imam.
Amesema masuala ya kiroho, mantiki na uadilifu ndio misingi mikuu ya mfumo wa Imam Khomeini. Amesema, Imam Khomeini alikuwa akitekeleza mambo hayo katika maeneno na matendo na kuongeza kuwa Imam alikuwa mtu wa dhikri, khushui, ucha-Mungu na takwa na alimtegemea Mwenyezi Mungu katika kila hali na wakati huo huo alitumia kikamilifu akili, busara, mahesabu na mantiki katika hali zote na kutekeleza uadilifu kutokana na mafundisho ya dini na Qur’ani.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa hatua ya kuchagua demokrasia ya kidini kama uwanja na medani ya mfumo wa kisiasa hapa nchini ni mfano wa mantiki na sera za kutumia akili za Imam Khomeini. Ameongeza kuwa kuegamia rai za wananchi na kushirikishwa taifa katika medani mbalimbali tena katika nchi ambayo ilikuwa ikitawaliwa kwa siasa za kiimla na kidikteta kwa karne kadhaa kunaonesha kwamba mantiki na kutumia akili katika kuongoza nchi ni sehemu muhimu ya mfumo unaotoa saada na ufanisi wa Imam Khomeini.
Ayatullah Khamenei amesema, kuwatambua maadui, kuwa macho na kusimama kidete kikamilifu mbele yao ni dhihirisho jingine la mantiki na kutumia akili kwa hayati Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu). Amesema, tofauti na baadhi ya watu ambao walikutambua kulegeza misimamo mbele ya maadui katika baadhi ya mambo kuwa ni uamuzi wa akili na busara, Imam Khomeini kwa kutegemea akili yake pevu, alikutambua kulegeza kamba na kurudi nyuma mbele ya maadui kuwa ni kuwapa fursa ya kusonga mbele; kwa sababu hiyo katika kipindi chote kilichojaa baraka cha uhai wake, Imam alisimama imara kama mlima mkabala wa maadui.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria suala la kuimarisha moyo wa kujiamini ndani ya roho ya taifa kuwa ni mfano mwingine wa akili na busara ya hayati Imam Khomeini (MA). Amezungumzia juhudi zilizofanywa na mabeberu na vibaraka wao wa ndani katika kipindi cha utawala wa Kajar na Pahlavi kwa ajili ya kueneza moyo wa kujihisi duni na dhaifu katika fikra za taifa la Iran na akasema: “Imam Khomeini alidunga roho ya kujiamini na kujitegemea katika taifa kama hilo na kutia kaulimbiu ya “Sisi Tunaweza” ndani ya nafsi zao.”
Katika uwanja huo Ayatullah Khamenei amesema kuwa maendeleo ya kustaajabisha ya vijana wasomi wa Iran katika nyanja mbalimbali za sayansi, teknolojia na viwanda ni matokeo ya juhudi za busara na mantiki ya Imam Khomeini kwa ajili ya kuhuisha uwezo wa taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mchakato wa kubuni katiba ni mfano mwingine wa fikra pevu na mantiki ya mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema, kwa kutumia mahesabu ya kina, Imam alilipa taifa jukumu la kuteua waandishi wa katiba mpya na baada ya kuandikwa, aliwapa wananchi wenyewe jukumu la kuipigia kura ya maoni.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, katika mfumo wa kifikra wa Imam Khomeini, wananchi ndio wamiliki halisi wa nchi. Ameongeza kuwa, kwa kutumia busara na mantiki, Imam aliwaambia wananchi kuwa wao ndio wamiliki wa nchi na si madikteta na viongozi wa tawala za kiimla ambao wakati wa utawala wa kidhalimu wa Shah, walijiona kuwa ndio wamiliki wa nchi.
Akikamilisha sehemu hii ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amesema, kwa hatua kama hizo za busara na mantiki, Imam Khomeini aliweka misingi imara ya kisheria, kijamii na kisiasa ya nchi ambayo inaweza kuwa nguzo na msingi imara wa ustaarabu adhimu wa Kiislamu.
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hadhara ya umati mkubwa wa wananchi waliofika katika haram ya Imam Khomeini katika siku ya kukumbuka tukio la kuaga dunia kiongozi hiyo, imeendelea kwa chunguza na kubainisha upande wa masuala ya kimaanawi na kiroho wa Imam kama moja ya nguzo kuu za mfumo wake.
Ayatullah Khamenei ameitaja ikhlasi kuwa ni dhihirisho la umaanawi na kushikamana barabara na masuala ya kiroho kwa Imam. Ameongeza kuwa tangu mwanzoni mwa mapambano yake Imam alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa moyo wa kuwajibika na daima alikuwa akiwausia viongozi wa dola kutekeleza wajibu na kazi zao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kuchunga masuala ya kiakhlaki na maadili mema ni mfano mwingine wa kushikamana na masuala ya kiroho na kimaanawi katika mfumo wa Imam Khomeini. Amesisitiza kuwa kujiepusha na dhambi, tuhuma, kusengenya, dhana mbaya, ghururi, majivuno na kadhalika ni suala ambalo Imam alishikimana nalo kikamilifu na daima aliwahimiza wananchi na viongozi kufuata njia hiyo.
Ayatullah Khamenei amesema, Imam daima alikuwa akiwausia viongozi wasijione kuwa juu zaidi ya wananchi wala kujiona kwamba hawana nakisi na kasoro za kukosolewa na wawe tayari kwa ajili ya kusikiliza ukosoaji na kueleza makosa yako.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, hatua ya Imam Khomeini ya kuashiria baadhi ya makosa yaliyofanyika hapa nchini inatokana na adhama ya roho ya shaskhsia huyo. Ameongeza kuwa darsa na somo kubwa la kiroho la Imam Khomeini kwa viongozi wote ni kwamba wasijione kuwa wana kinga ya kufanya makosa.
Akibainisha uadilifu kama sehemu nyingine ya misingi muhimu ya mfumo wa Imam Khomeini, Ayatullah Khamenei ameashiria mwenendo wa Imam wa kuwajali watu wa tabaka la chini na kusema Imam alisisitiza mno juu ya udharura wa kushughulikiwa watu wa matabaka dhaifu na daima aliwahimiza viongozi kujiepusha na tabia za kibwanyenye na kuwataka wawasaidie watu maskini na wa tabaka la chini. Ayatullah Khamenei amesema somo hilo kubwa halipaswi kusahauliwa katika hali yoyote.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kufuatilia maisha ya hali ya juu ya mtu binafsi na kujikusanyia utajiri na mali ni maradhi makubwa kwa viongozi wa dola. Ameongeza kuwa Imam alijiweka mbali kabisa na maradhi hayo na alikuwa akiwataka viongozi kuwa pamoja na wananchi na kuwa karibu yao.
Ameashiria pia sisitizo la Imam Khomeini la kuchaguliwa viongozi kutoka kwenye tabaka la wananchi wa kawaida na kusema, Imam alipinga suala la kutambuliwa uhusiano wa kifamilia na kuwa karibu na watu mashuhuri kama kigezo cha mtu kupewa mamlaka ya uongozi na alikuwa akisema kuwa kutegemea nguvu na mali kwa ajili ya kuchukua mamlaka na uongozi ni hatari kubwa mno.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kushikamana na mfumo wa Imam Khomeini kunalipa taifa heshima ya kitaifa na hadhi ya kimataifa. Amesisitiza tena juu ya udharura wa kutazamwa pande zote za mfumo wa Imam na akasema kuwa iwapo mtu au mrengo wowote utatupilia mbali thamani kwa kisingizio cha kushikamana na hekima na akili au ukalegeza kamba mbele ya adui kutokana na kughafilika na njama na hadaa zake, basi mtu au mrengo huo utakuwa umepotea na kulisaliti taifa.
Amesema kuwa kupuuza upande wa masuala ya kiroho na kimaadili wa Imam Khomeini kwa kisingizio cha kupigania uadilifu na misimamo ya kimapinduzi ni kutoka nje ya mfumo wa Imam. Amesisitiza kuwa iwapo tutawadhalilisha, kuwaudhi na kuwakera ndugu waumini na watu ambao kimsingi wana imani na mfumo na utawala wa Kiislamu na Uislamu lakini wanatofautiana nasi kifikra, basi tutakuwa tumetoka nje ya njia ya Imam.
Katika uwanja huo, Ayatullah Ali Khamenei amesema iwapo tutawanyima usalama baadhi ya watu kwa kisingizio cha kuwa wanamapinduzi, hicho pia kitakuwa kielelezo cha kupotoka na kuondoka katika njia ya Imam.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uaminifu kamili wa taifa la Iran na kushikamana kwake na njia ya Imam Khomeini, istiqama na kutekeleza majukumu ya kitaifa ya kulinda na kuimarisha thamani aali na akasema kuwa adui alikuwa akidhani kuwa kufariki dunia Imam Khomeini utakuwa mwanzo wa kusambaratika utawala wa Kiislamu nchini Iran, lakini mshikamano na mahudhurio makubwa ya wananchi wakati wa mazishi ya Imam Khomeini na misimamo imara ya wananchi ya kuunga mkono maamuzi yaliyochukuliwa na Baraza la Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu wa Nchi viliwakatisha tamaa maadui ambao walianza kupanga mikakati ya kipindi cha miaka kumi.
Ameashiria matukio ya mwaka 1378 Hijria Shamsia yaani miaka kumi baada ya kufariki dunia Imam Khomeini na kusema, tarehe 23 Tir 1378 wananchi wote walibatilisha njama na mipango yote iliyokuwa imepangwa na adui kwa kipindi cha miaka kumi.
Ayatullah Khamenei ameashiria mikakati ya kipindi kingine cha miaka kumi ya maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema kuwa maadui walidhani kwamba mwaka 1388 Hijria Shamsia kulikuwa na fursa nzuri ya kutekeleza njama zao na kwamba wanaweza kutekeleza njama hizo kwa kutilia maanani matakwa ya wananchi wafuasi wa utawala wa Kiislamu; hata hivyo baada ya vuguvugu la miezi miwili hadi mitatu mjini Tehran wananchi waling’amua uhakika wa mambo katika Siku ya Kimataifa ya Quds na siku ya Ashura na wakakomesha kabisa fitina hiyo tarehe 9 Dei. Amesisitiza kuwa katika siku zijazo pia wananchi wa Iran wataendeleza njia hiyo yenye nuru na mwanga kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na mwamko, azma, imani na irada yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mahudhurio makubwa ya wananchi katika medani mbalimbali yanalinda amani na usalama wa nchi na kubatilisha njama za maadui. Amezungumzia kazi kubwa za miundombinu zilizofanyika hapa nchini na kusema, kwa matakwa yake Mola, wananchi wataona matunda ya kazi hizo katika kipindi cha muda mfupi na kipindi cha muda mrefu.
Ayatullah Khamenei amesema, kuwepo wasomi vijana wa Iran katika daraja za juu za medani mbalimbali za sayansi na elimu duniani ni miongoni mwa matunda ya mshikamano na hali ya kuaminiana inayoshuhudiwa kati ya wananchi na viongozi wao hapa nchini. Amesema kuwa kadiri wananchi wanavyohudhuria na kushiriki kwa wingi katika medani mbalimbali na hali ya kuaminiana kati ya taifa na viongozi ikaimarika zaidi basi hapana shaka kwamba malengo ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu na maendeleo ya nchi yatashika kazi zaidi.
Sehemu ya pili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika shughuli ya kukumbuka mwaka wa 22 tangu Imam Khomeini afariki dunia imechunguza masuala ya kieneo.
Ameutaja mwamko mkubwa wa Kiislamu huko kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati kuwa ni muhimu wa ya kihistoria. Amesema kuwa kila moja kati ya matukio ya Misri, Tunisia, Libya, Yemen na Bahrain lina uchambuzi na hukumu yake lakini pale taifa linapoamka na kujihisi kuwa na nguvu na uwezo, hakuna kitu kinachoweza kulizuia kufikia ushindi.
Amesema kuwa mfumo wa ubeberu, Shetani Mkubwa (Marekani) na Wazayuni makatili wanafanya njama za kuzuia ushindi wa mwisho wa mataifa ya maeneo hayo, lakini iwapo mataifa yaliyoamka yatasikia wito wa Qur’ani wa kuwa na subira, kusimama kidete na kuwa na imani na ahadi ya Mwenyezi Mungu hapana shaka kwamba yatapata ushindi.
Ayatullah Khamenei amesema, siasa na mipango ya nchi za Magharibi huko Libya ni kuanzisha nchi dhaifu na isiyokuwa na nguvu. Ameongeza kuwa Libya ni nchi muhimu na yenye utajiri wa maliasili ya mafuta ambayo ni jirani na Ulaya, kwa msingi huo Wamagharibi wanataka kuidhoofisha nchi hiyo kwa kuanzisha vita vya ndani ili baadaye waweze kuidhibiti kwa njia ya moja kwa moja au isiyokuwa ya moja kwa moja.
Amesema hali ya Yemen inashabihiana na ile ya Libya. Kuhusu Bahrain, Ayatullah Khamenei amesema wananchi wa Bahrain wako chini ya dhulma kubwa na Wamagharibi na washirika wao wanataka kuidhihirisha harakati ya wananchi wa Bahrain kuwa ni ya kimadhehebu kwa kuipachika jina la harakati ya Kishia. Amesema ni kweli kwamba katika kipindi chote cha historia asilimia kubwa ya wananchi wa Bahrain walikuwa na ni Waislamu wa madhehebu ya Shia lakini kadhia ya Bahrain si suala la Shia na Suni bali ni kadhia ya taifa linalodhulumiwa ambalo linadai haki zake za kimsingi, yaani haki ya kupiga kura na kushirikishwa katika uundaji wa serikali.
Ayatullah Khamenei amesema: “Wamarekani warongo na laghai wanashiriki vilivyo katika kukandamiza wananchi wa Bahrain licha ya madai yao ya kutetea haki za binadamu na demokrasia. Pamoja na hayo wanasema, Wasaudi Arabia wamekwenda Bahrain, ilhali watu wote wanaelewa kwamba Wasaudia hawawezi kuchukua hatua hiyo bila ya idhini ya Marekani; kwa msingi huo Wamarekani pia wanahusika katika kadhia ya Bahrain.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa harakati za wananchi katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika zinakutana katika sifa kuu tatu ambazo ni kuwa zote “ni za Kiislamu”, ni “dhidi ya Marekani na Wazayuni” na “ni za wananchi”. Ameongeza kuwa sifa hizo zinaonekana waziwazi hususan katika mapinduzi ya wananchi wa Misri.
Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaunga mkono harakati yoyote inayofanyika ikiwa na sifa hizo na itakapoona kuwa harakati hizo zinachochewa na Marekani na Wazayuni, basi haitaziunga mkono, kwani inaamini kwamba Shetani Mkubwa Marekani na waitifaki wake hawafanyi jambo lolote lenye maslahi kwa mataifa.
Ayatullah Khamenei ameyataka mataifa ya kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati kuwa macho mbele ya harakati za Magharibi na akasema, misaada inayotolewa na Marekani ni miongoni mwa njia zinazotumiwa kwa ajili ya kuyadhibiti mataifa mbalimbali, kwa msingi huo mataifa ya eneo hili hususan taifa la Misri lenye urithi tajiri wa Kiislamu na kiutamaduni, yanapaswa kuwa macho ili dui aliyeondoka kupitia mlangoni asije akarudi kwa kupitia dirishani.
Amepongeza harakati kubwa ya wananchi wa Misri kuhusu suala la Palestina, Ukanda wa Gaza na kivuko cha Rafah na akasema, kuna udharura wa kudumishwa harakati kama hizo ili malengo ya wananchi wa Misri yakamilike kwa baraka zake Mwenyezi Mungu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena juu ya udharura wa kuwa macho mbele ya njama za mfumo wa kibeberu za kutaka kuanzisha ufa na mgwawanyiko kati ya Mataifa ya Mashariki ya Kati na taifa la Iran na akasema, katika baadhi ya nchi ikiwemo Misri, mawahabi na makundi yanayowakufurisha Waislamu yanafanya jitihada za kuzusha hitilafu kati ya wananchi, kwa msingi huo tahadhari inapaswa kuchukuliwa.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia kadhia ya Palestina na kusema kuwa Palestina haiwezi kugawanywa na ardhi yote ya nchi hiyo ni mali ya Waislamu. Amesisitiza kuwa hapana shaka kwamba Palestina itarejea katika mikono ya Uislamu.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa ufumbuzi unaotolewa na Wamarekani kwa ajili ya kadhia ya Palestina hautazaa matunda na suluhisho la kadhia hiyo ni lile lililopendekezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran miaka kadhaa iliyopita ambalo kwa mujibu wake, aina ya serikali itakayoongoza ardhi zote za Palestina inapaswa kuainishwa katika kura ya maoni itakayowashirikisha wananchi wote wa Palestina.
Ameongeza kuwa baada ya kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi katika ardhi yote ya Palestina, taifa la Palestina litachukua uamuzi kuhusu Wazayuni waliovamia nchi hiyo kutoka nje. 803396



captcha