Akizungumza leo Ijumaa, Jonathan amesema magaidi wa Boko Haram wanazidi kuhoofika siku hadi siku.
Wakati huo huo, msemaji wa serikali ya Nigeria, Mike Omeri amesema kuwa nchi hiyo imeanzisha shambulizi la mwisho la kijeshi dhidi ya kundi la Boko Haram. Omeri amesema kuwa katika wiki za hivi karibuni jeshi la nchi hiyo limepata mafanikio muhimu dhidi ya kundi la Boko Haram. Ameongeza kuwa maeneo manne ya Borno ambayo ni Bama, Abadam, Gwoza na Askira ndiko ambako kundi hilo la kigaidi na kitakfiri lingali linaendesha shughiuli zake na kwamba maeneo hayo ndiyo yaliyodhurika zaidi kutokana na harakati za Boko Haram.
Inasemekana kuwa jeshi la Nigeria katika siku za kati ya Ijumaa na Jumatatu iliyopita, lilifanikiwa kukomboa majimbo mawili ya Yobe na Adamawa ambayo yalikuwa yakisumbuliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Boko Haram. Msemaji wa serikali ya Nigeria amesema miji 36 imekombolea na jeshi la nchi hiyo tangu yalipoanza mashambulizi dhidi ya kundi hilo la kigaidi mwishoni mwa mwezi Januari. Lengo la mashambulizi ya mwisho kabisa ya jeshi la Nigeria dhidi ya kundi hilo la kigaidi limetajwa kuwa ni kuliangamiza kikamilifu. Kundi hilo pia limekuwa likivuruga usalama na amani katika nchi jirani na Nigeria kama Cameroon, Niger na Chad.
Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa kuzidishwa mashambulizi ya jeshi la Nigeria dhidi ya Boko Haram katika kipindi hiki cha kukaribia uchaguzi mkuu nchini humo kunatia shaka kubwa. Utendaji mbaya wa Rais Godluck Jonathan katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni unatatiza kampeni yake ya kugombea tena kiti hicho. Mgogoro wa kiuchumi, ongezeko la umaskini na ukosefu wa ajira sambamba na machafuko ya kisiasa vyote kwa pamoja vimepunguza sana umaarufu wa kiongozi wa sasa wa serikali ya Abuja.
Wakati huo huo harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram zinawahamasisha zaidi Wanigeria kutaka mabadiliko ya kisiasa nchini kwao. Uzembe wa serikali ya Godluck Jonathan katika kukabiliana na mashambulizi kundi hilo la kigaidi umekuwa na taathira kubwa katika kampeni za uchaguzi wa rais wa nchi hiyo. Hii ni pamoja na kuwa Wanigeria bado hawajasahau maafa ya kutekwa nyara wasichama 275 wa shule ambao walichukuliwa na wapiganaji wa Boko Haram na hadi sasa serikali ya nchi hiyo haijaweza kuwakomboa.
Kushadidi kwa mashambulizi ya kundi hilo la kitakfiri kumewafanya hata baadhi ya shakhsia wa Nigeria waamini kwamba, serikali inashirikiana nao kwa njia moja au nyingine. Baadhi ya wakosoaji wanasema Rais Jonathan ameruhusu kundi hilo kuendeleza machafuko na migogoro katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo yenye idadi kubwa ya Waislamu ili kupunguza idadi yao katika masanduku ya kupigia kura.../mh