
Jumamosi, tawi la New York la Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Wamarekani (CAIR-NY) liliukaribisha msimamo wa Columbia University wa kulaani tukio hilo lililolenga Muislamu kwa chuki ya kidini.
Bi. Claire Shipman, Rais wa muda wa Chuo Kikuu cha Columbia, alisema: "Wiki iliyopita, nje ya lango letu, mmoja wa wanafunzi wetu alikumbana na hali ya kutisha na ya kusikitisha. Mtu asiye na uhusiano na Chuo alimkejeli mwanafunzi wetu kwa misingi ya utambulisho wake. Alitoa maneno ya dharau kuhusu niqab ya mwanafunzi wetu na kisha kumfuata barabarani… Tukio hili limepelekwa kwa Polisi wa NYPD kuchunguzwa kama uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu. Ijapokuwa lilitokea nje ya lango letu, ni wazi: hatuna nafasi kwa aina hii ya chuki katika Columbia. Chuki dhidi ya Waislamu, chuki dhidi ya Waarabu, ndani au nje ya kampasi, haikubaliki kabisa."
Afaf Nasher, Mkurugenzi Mtendaji wa CAIR-NY, alisema: "Tunakubaliana kikamilifu na ujumbe thabiti kwamba chuki dhidi ya Waislamu na Waarabu haina nafasi katika Chuo Kikuu cha Columbia wala katika jiji letu. Tunakaribisha kulaaniwa kwa dhahiri kwa tukio hili la chuki lililomlenga dada Muislamu karibu na kampasi. Hakuna mwanafunzi anayepaswa kutishwa au kudhalilishwa kwa sababu ya imani yake au namna anavyoichunga."
Hata hivyo, Nasher aliongeza kuwa: "Ni lazima tutambue kwamba matukio ya chuki hayajitokezi kwa bahati mbaya. Chuo Kikuu cha Columbia kama taasisi imewadhulumu Waislamu na Waarabu kwa shughuli za maandamano ya amani kuhusu Palestina. Taasisi kubwa zinapotumia nguvu zao kuumiza kwa dhulma, watu binafsi hujipa ujasiri wa kutenda kwa uovu sawa. Tunatumai dada huyu Muislamu na wanafunzi wengine waliolengwa katika miaka miwili iliyopita hawataendelea kuishi katika hali hizi za kudhalilisha."
CAIR ilibainisha kuwa mwaka jana iliweka Chuo Kikuu cha Columbia katika orodha ya “taasisi za wasiwasi maalum” kutokana na ukatili wake dhidi ya waandamanaji wa kupinga mauaji ya halaiki.
Aidha, mapema mwezi huu, CAIR-NY ilionyesha kuwa mashambulizi ya mtandaoni yenye chuki za Kiislamu na za kibaguzi kuhusiana na uchaguzi wa Meya wa New York yalikuwa kampeni ya kimfumo ya kuwadhalilisha Waislamu na wageni.
CAIR-NY pia ililaani tukio la chuki dhidi ya Waislamu na kupinga Palestina lililowalenga wanandoa wa Kiirani na Kipalestina ndani ya treni ya chini ya ardhi ya New York.
Ripoti ya Haki za Kiraia ya CAIR ya mwaka 2025, Unconstitutional Crackdowns, imeonyesha kuwa kiwango cha Chuki Dhidi ya Uislamu au Islamophobia kimefikia rekodi ya juu kote nchini Marekani.
3495413