IQNA

Kituo cha uchapishaji wa Qur'ani Tukufu Iran chatumia Teknolojia ya Akili Mnemba

17:07 - November 09, 2025
Habari ID: 3481490
IQNA – Kituo cha Uchapishaji na Usambazaji wa Qur'an Tukufu cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimeanza kutumia teknolojia za Akili Mnemba (AI) kwa ajili ya kutengeneza nakala za Qur'ani za kidijitali, hatua inayofungua ukurasa mpya wa kuunganisha urithi wa kiroho na ubunifu wa kisasa.

Kituo hiki kilianzishwa mwaka 1994 kwa amri ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kinatambulika rasmi kama mamlaka ya kitaifa ya uchapishaji wa Qur'ani Tukufu nchini Iran. Kwa takriban miaka thelathini, kimekuwa kikiunganisha kaligrafia ya kitamaduni na teknolojia ya kidijitali ili kuendeleza uchapishaji, utafiti, na uhifadhi wa Qur'an Tukufu.

Akizungumza na IQNA, Hadi Ebadi, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Vyombo vya Mawasiliano katika kituo hicho, alisema kuwa matumizi ya akili mnemba yanalenga kufanya uchapishaji wa Qur'ani kuwa wa kibinafsi zaidi na wa mwingiliano wa moja kwa moja.

Alifafanua, “Lengo letu kuu ni kuchapisha nakala za Qur'ani Tukufu zinazotumia akili mnemba ambazo zitabuniwa kwa mahitaji ya kila msomaji , ambapo mtumiaji ataweza kuchagua aina ya maandishi, mpangilio wa kurasa, rangi, tafsiri, na hata mtindo wa kisomo.”

Ebadi alibainisha kuwa tafiti za awali kuhusu mradi huu tayari zimeanza kwa ushirikiano na kampuni za kitaalamu za kiteknolojia.

“Teknolojia hii inapaswa kuelewa muundo wa maandiko ya Qur'an, kuchagua alama sahihi za matamshi, na kuweza kuendana na riwaya mbalimbali za kisomo,” alisema, akiongeza kuwa mfano wa awali wa nakala hiyo Qur'ani unaweza kuzinduliwa katika miaka ijayo.

Ubunifu wa kituo hiki ulianza mapema miaka ya 2000 kwa kutengeneza aina ya kwanza duniani ya maandishi ya Qur'an yenye akili mnemba.

Aina hiyo ya maandishi, iliyobuniwa kati ya mwaka 2003 na 2004, iliweza kurekebisha herufi kiotomatiki, kutumia kanuni za kitaalamu za alama za matamshi, na kuiga usahihi wa kaligrafia ya Qur'an ya kitamaduni. “Ilikuwa kama kaligrafia ya mtandaoni,” Ebadi alisema.

Mbali na ubunifu wa uchapishaji, kituo hiki pia kinaendesha mradi wa kidijitali uitwao Kwenye Fuko la Aya, unaowasilisha aya za Qur'an kila siku pamoja na kisomo, tafsiri, na riwaya zinazohusiana.

Ebadi alielezea mradi huo kama “daraja kati ya utafiti wa kitaaluma na umma,” unaolenga kuimarisha tafakuri ya Qur'an na kuonyesha urithi wa karne nyingi wa hati za Kiislamu.

3495322

captcha