Ayatullah Naser Makarem Shirazi alitoa kauli hiyo Jumatano wakati wa kikao na rais, watafiti na wanazuoni wa Qur’ani Tukufu kutoka Kituo cha Noor cha Utafiti wa Kompyuta na Sayansi za Kiislamu.
Mkutano huo ulikuwa wa utambulisho wa jukwaa jipya lenye uwezo wa akili mnemba lijulikanalo kama “Chat with Tafasir”, lililobuniwa kusaidia watumiaji kutafuta na kujadili tafsiri za Qur’ani Tukufu.
Ayatullah Makarem Shirazi alisifu mafanikio ya kituo hicho na kusisitiza kuwa hawajasalia nyuma katika masuala ya sayansi na teknolojia. Badala yake, wamekuwa mstari wa mbele katika kutumia akili mnemba (Artificial Intelligence) kwa ajili ya Qur’ani Tukufu na mafundisho ya Ahlul-Bayt (AS).
Akinukuu maneno ya Nahj al-Balagha, alisema:
“Hakika Mwenyezi Mungu hajamnasihi mtu kwa kitu chochote kama alivyomnasihi kwa Qur’ani… Ndani yake kuna chemchemi ya moyo na vyanzo vya maarifa, na hakuna kinachotakasa moyo isipokuwa Qur’ani.”
Alifafanua kuwa Qur’ani ni chemchemi ya maarifa na kipimo cha kutofautisha kati ya haki na batili. Kila muumini anapoitazama, uelewa huongezeka na ujinga hupungua.
Marja huyo pia alinukuu aya ya Qur’ani (16:89):
“Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinachobainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu.”
Alisema kuwa aya hiyo inaashiria kwamba Qur’ani imebeba mwongozo unaohitajika kwa maisha ya mwanadamu. “Iwapo hatulioni jambo ndani ya Qur’ani, basi upungufu uko katika uelewa wetu, siyo katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu,” aliongeza.

Ameeleza pia kuwa tafsiri za Qur’ani (tafsir) hapo awali hazikuonekana kama taaluma ya kisayansi, lakini leo zinatambuliwa kama fani iliyo na misingi madhubuti, ikiwemo uchambuzi wa lugha, utafiti wa muktadha na uchunguzi wa maana kwa kina. Akasema akili mnemba inaweza kufanya kazi hizi kwa usahihi, kwa kasi kubwa na kwa uwezo mpana wa kuhifadhi taarifa.
Kadhalika, alihimiza kuongezwa kwa juhudi za kuufahamisha umma kuhusu mafanikio ya kiteknolojia ya taasisi za Kiislamu. Alisema miradi mingi yenye thamani haijulikani vya kutosha, na vyombo vya habari vina wajibu wa kuonyesha jinsi seminari za Kiislamu zinavyopiga hatua katika sayansi na teknolojia. Kueneza taarifa hizo, alisisitiza, kutachochea utafiti zaidi.
Akirejea amri ya Qur’ani katika aya (8:60):
“Basi waandalieni nguvu kadiri muwezavyo…” Alibainisha kwamba dhana hiyo leo inahusisha si tu maandalizi ya kijeshi bali pia nguvu katika nyanja za kitamaduni na kielimu. “Leo mapambano ni ya kitamaduni, na lazima tujihami kwa zana za kisayansi na akili bandia,” aliongeza.
Mwisho, Ayatullah Makarem Shirazi alieleza matumaini kuwa matumizi ya akili mnemba yatazidi kuimarisha mchango wake katika taaluma za Kiislamu kama vile tafsiri, fiqhi, usul al-fiqh na tarikh.
3495390