
Waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya Kenya walikusanyika Jumamosi katika Bustani ya Uhuru kwa tukio kubwa la upandaji miti lililoandaliwa na kundi la Voices for Palestine. Tukio hilo, ambalo pia liliendelea hadi Bustani ya Kati (Central Park), lililenga kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina na kuadhimisha zaidi ya karne moja tangu kutolewa kwa Tamko la Balfour la Novemba 2, 1917, tukio linaloonekana na wengi kama chanzo cha mateso ya Wapalestina.
Tamko hilo lililenga kuendeleza na kuimarisha harakati za Uzayuni, na hatimaye likapelekea kuporwa kwa ardhi za Palestina na kuundwa kwa utawala haramu wa Israel, ambao wengi wanauona kuwa haramu.
Waandaaji na washiriki walipanda miti 10,000 kama alama ya ukumbusho, muqawama (mapambano ya kimaanawi), na uamsho wa matumaini. Miti hiyo inalenga kuwa kumbukumbu hai ya Wapalestina waliopoteza ardhi zao za jadi, waliokumbwa na uvamizi, na wanaoendelea kuathiriwa na ukatili wa utawala wa Israel. Mpango huu pia unaunga mkono lengo la kitaifa la Kenya la kuongeza uoto wa asili na kurejesha bustani za umma.
Akihutubia hadhara, Sheikh Badru Jaffar wa Msikiti wa Jamia Nairobi alisema mkusanyiko huo ni hatua ya maadili na mazingira. Alieleza kuwa upandaji miti hauhusu tu uhifadhi wa mazingira, bali pia ni wito wa haki na amani duniani.
“Hili si suala la kupanda miti tu; ni wito wa kimataifa wa haki,” alisema Sheikh Badru katika Bustani ya Uhuru.
Kwa mujibu wa waandaaji, tarehe ya Novemba 2 ilichaguliwa kwa makusudi ili kuambatana na kumbukumbu ya Tamko la Balfour. Walisema kuwa kwa kupanda miti katika siku hii, washiriki waliunganisha juhudi za mazingira za Kenya na harakati za kimataifa za haki za binadamu.
Tukio hilo pia lililenga kuongeza uelewa kuhusu migogoro ya kibinadamu inayoendelea katika Ukanda wa Gaza na maeneo mengine ya Palestina. Washiriki wengi walibeba mabango na plakadi zenye ujumbe wa amani na haki, huku wengine wakitoa dua kwa ajili ya wahanga wa mzozo unaoendelea.
Tangu Oktoba 2023, utawala dhalimu wa Israel ulianzisha mauaji ya kimbar dhidi ya Gaza kwa kiwango cha kutisha. Kwa mujibu wa takwimu kutoka mashirika ya kibinadamu, zaidi ya Wapalestina 69,000 wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Mashirika hayo pia yameeleza wasiwasi kuhusu uhaba mkubwa wa chakula, dawa, na maji safi, pamoja na uharibifu wa hospitali, shule, na makazi ya raia.
Makubaliano ya kusitisha vita kati ya utawala wa Israel na Hamas yalifikiwa Oktoba 10 kufuatia juhudi za upatanisho zilizojikita katika mpango wa amani wa vipengele 20. Hata hivyo, makubaliano hayo yamekiukwa mara kadhaa, na kusababisha vifo zaidi na kurejea kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Waandaaji wa Voices for Palestine wanasema kuwa tukio la Bustani ya Uhuru pia lililenga kuonyesha uhusiano kati ya haki ya mazingira na haki za binadamu. Walibainisha kuwa changamoto za kimazingira kama ukataji miti na uchafuzi wa mazingira huathiri zaidi jamii zilizo hatarini—ikiwemo zile zinazokumbwa na vita.
Washiriki walieleza matumaini yao kuwa miti iliyopandwa itakua na kuwa alama ya kudumu ya amani na ustahimilivu. Wengi walisisitiza kuwa haki kwa Palestina inapaswa kuwa kipaumbele cha kimataifa, si suala la kisiasa au kikanda pekee.
Sheikh Badru na viongozi wengine wa kidini walihimiza ushiriki endelevu kutoka kwa Waislamu wa Kenya na jamii kwa ujumla katika ujenzi wa amani na kazi za kibinadamu. Walihamasisha wananchi kushiriki katika juhudi zinazochanganya imani, maadili, na uwajibikaji wa kijamii.



/3495244