
Kila siku, wasomaji wa Qur'ani waliobobea hukusanyika katika sehemu maalum ya kasri hiyo, wakisoma Qur'ani kwa sauti ya utulivu na kwa tajwidi ya hali ya juu. Usomaji huu unafanyika kwa zamu, kuhakikisha kuwa Qur'ani inasomwa bila kukatizwa, mchana na usiku, kama ishara ya heshima na ibada ya kudumu.
Kasri ya Topkapi, ambayo ilikuwa makazi ya kifalme ya Masultani wa Uthmaniyya kwa karne nyingi, ina sehemu maalum ya hifadhi ya Qur'ani na maandiko mengine ya Kiislamu. Usomaji huu wa Qur'ani unahusishwa na baraka za mahali hapo, na unachukuliwa kama ibada ya kudumu inayowakumbusha Waislamu umuhimu wa kuendeleza mafunzo ya Qur'ani katika maisha ya kila siku.
Qur'ani Tukufu husomwa bila kukoma katika Kasri ya Topkapı jijini Istanbul na mhafidh 28 waliohifadhi Qur'ani nzima. Kila Hafidh husoma kwa zamu ya dakika 45 hadi saa moja, mchana na usiku, kwa mfumo wa kupokezana unaohakikisha usomaji endelevu. Kwa utaratibu huu, hatma moja ya Qur'ani hukamilika kila siku, na hivyo kufikia hatma 365 kwa mwaka.
Desturi hii ya kiroho ilianzishwa wakati wa utawala wa Yavuz Sultan Selim, ambaye aliongoza kundi la mahafidh 40 katika usomaji wa Qur'ani. Tangu wakati huo, utamaduni huu umehifadhiwa kwa heshima na uaminifu mkubwa.
Baada ya kampeni ya Misri ya mwaka 1517, masalio matakatifu yaliletwa Istanbul na kuhifadhiwa kwa uangalifu mkubwa katika chumba cha "Amanat Muqaddasa" ndani ya Kasri ya Topkapı kwa zaidi ya miaka 500. Miongoni mwa masalio hayo ni Vazi Tukufu la Mtume Muhammad (SAW) , "Hırka-i Saadet", barua zake, upanga wake, jino lililovunjika katika vita vya Uhud, nywele zake tukufu , "Sakal-ı Sharif", na alama ya nyayo zake.
Chumba hicho pia kinaonyesha mapanga ya makhalifa na masahaba wa Mtume (SAW), funguo za Kaaba, na sanduku la jiwe jeusi, "Hajar al-Aswad", vyote vikiwa na umuhimu mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ilhan Kocaman, mkuu wa idara ya Kasri ya Topkapı, alisema kuwa kasri hiyo ni kiini cha kihistoria cha Istanbul, na kwamba masalio ya thamani kutoka maeneo mbalimbali yaliletwa hapo wakati wa utawala wa Uthmaniyya. Alifafanua kuwa kwa kuwa Istanbul ilikuwa makao ya ukhalifa, masalio hayo matakatifu yalihifadhiwa hapo kwa heshima.
"Wakati Sultan Selim aliteka Hijaz na Misri, alileta ukhalifa pamoja na turathi za kitamaduni zinazonasibishwa na Mtume Muhammad (SAW) hadi Istanbul," alisema Kocaman. "Sultan Selim alisema, ‘Nitafutieni mahafidh 39, nami nitakuwa wa 40.’ Usomaji wa Qur'ani wa saa 24 ulianza siku hiyo na unaendelea hadi leo."
Kocaman alieleza heshima ya Wauthmaniyya kwa mabaki hayo ya kitamaduni na kuongeza kuwa hata vumbi lililokusanywa wakati wa kusafisha chumba cha Vazi Tukufu halikutupwa, bali lilihifadhiwa katika kisima maalum. "Hii inaonyesha heshima waliyoitoa mababu zetu kwa vitu vilivyobaki vya Mtume (SAW) na vitu vingine vitakatifu," alisema.
Aliifananisha Kasri ya Topkapı na Madina, mji alioishi Mtume Muhammad (SAW), akisisitiza uwepo wa Vazi Tukufu, jino lililovunjika, masalio ya manabii wengine, na vitu vya Ahlul Bayt (familia ya Mtume Muhammad SAW) ndani ya chumba hicho. Wageni wanaingia kwa kufuata taratibu kali za heshima.
Kuhusu usomaji wa Qur'ani unaoendelea, Kocaman alisisitiza kuwa kasri hiyo inachukulia jukumu lake kama mrithi wa utamaduni huu kwa uzito mkubwa. Usomaji wa moja kwa moja ulioanza wakati wa utawala wa Sultan Selim unaendelea kwa fahari na uaminifu.
Wageni mara nyingi husikia usomaji wa Qur'ani kutoka nje ya chumba na hudhani ni rekodi. Lakini wanapoingia na kuwaona maḥfiẓi wakisoma kwa macho yao, uzoefu wao huwa wa kipekee. "Watu wa kila asili , wenyeji, wageni, Waislamu na wasio Waislamu, husikiliza kwa makini na heshima," alisema.
Halil Ibrahim Akgün, mmoja wa maḥafidh wanaosoma Qur'ani hapo, alisema kuwa mapenzi ya taifa kwa Mtume Muhammad (SAW), yanayoitwa "‘Ishq-i Muhammadi", yanaonekana katika kazi yao. Alieleza kuwa kuhudumu katika sehemu hiyo tukufu ni dhihirisho la wazi la mapenzi na uaminifu huo.
Akgün alisema kuwa wakati wa huduma yake, alihisi hisia ambazo ni vigumu kuelezea kwa maneno. "Sisi ni daraja kati ya zamani na yajayo," alisema. "Tunajaribu kutekeleza amana hii, iliyotufikia kutoka kwa mababu zetu na Sultan Yavuz Selim, kwa heshima kubwa. Amana hii itarithiwa na vizazi vitakavyokuja."
Alihitimisha kwa kusema kuwa utamaduni huu wa karne tano bila kukoma ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. "Ni fadhila kutoka kwa Allah. Tunajivunia kuwa sehemu ya utamaduni huu na kuhudumu hapa usiku na mchana. Ninashukuru na najihisi mnyenyekevu kwa heshima hii," alisema.
Kwa Waislamu wa Pwani ya Afrika Mashariki, utamaduni huu wa usomaji wa Qur'ani bila kukoma unalingana na desturi za madrasa, khitma, na halaqa zinazofanyika katika misikiti ya kihistoria kama vile Msikiti wa Malindi, Lamu, na Kilwa. Ni ushahidi wa jinsi Qur'ani inavyodumishwa kama nuru ya maarifa na ibada katika jamii za Kiislamu.
3495292