IQNA

Kikao cha Sharjah kuhusu maandishi ya Qur'ani Tukufu katika dunia ya kidijitali

15:37 - November 16, 2025
Habari ID: 3481525
IQNA – Je, ni vipi maandishi ya kidini kama Qur’ani Tukufu  yanaweza kuthibitishwa kuwa sahihi na kusomwa kwa kutumia akili mnemba (AI) ya kisasa?

Hili ndilo swali kuu lililojadiliwa katika kongamano maalum wakati wa Maonyesho ya Vitabu ya Kimataifa ya Sharjah 2025, ambapo wasomi walitoa wito wa mabadiliko ya kimsingi.

Kongamano hilo, lenye mada “Utunzaji wa Kisayansi: Mtazamo Asilia kwa Maono ya Kisasa”, liliandaliwa na Chuo cha Qur’ani Tukufu Sharjah kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Mohamed bin Zayed cha Binadamu, Chuo Kikuu cha Sharjah, na Chuo Kikuu cha Al Qasimia.

 Washiriki walisisitiza haja ya kuendeleza viwango vipya na kutumia zana za kiteknolojia za kisasa kwa uthibitishaji wa kitaaluma, sambamba na kuweka misingi ya kimbinu kwa vyuo vikuu na majukwaa ya utafiti ili kuhakikisha maandiko yanazalishwa na kuthibitishwa kwa mujibu wa viwango sahihi vya kimataifa.

Mapendekezo ya kongamano yalihimiza matumizi ya akili mnemba au AI kama msaidizi wa utafiti, kwa kufuata mbinu zinazotambulika kimataifa za uthibitishaji. Pia yalitaka ushirikiano wa kina kati ya taasisi za kielimu na utafiti ili kubadilishana maarifa na data, kuanzisha miradi ya pamoja, kuchunguza vipengele vipya katika tafiti za kiisimu za Qur’ani, na kuboresha tafsiri ili kulinda urithi tajiri wa Qur’ani.

Dkt. Abdullah Khalaf Al-Hosani, Katibu Mkuu wa Chuo cha Qur’ani Tukufu Sharjah, alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na vyuo vikuu vinavyotambulika kitaifa na kimataifa.

Kongamano hili liliwaleta pamoja wataalamu kutoka vyuo shiriki kujadili masuala ya Qur’ani, likibainisha kuwa teknolojia za kisasa, uthibitishaji wa kimbinu na nidhamu ya kitaaluma ni nguzo muhimu za kuhifadhi urithi wa kitamaduni na kuendeleza utafiti wa kielimu kwa vizazi vijavyo.

Mada kuu tatu zilizojadiliwa ni:

  • Mbinu za uthibitishaji wa kisayansi
  •  Uthibitishaji katika qira’a za Qur’ani na sayansi zinazohusiana
  •  Uhakika wa maandiko ya kisayansi katika enzi ya akili mnemba

3495410

Kishikizo: sharjah qurani tukufu
captcha