
Mashindano haya, yaliyofanyika katika mji wa Hamedan, upande wa magharibi mwa Iran, yalifanyika kuanzia Novemba 11 hadi 14 na yamejumuisha zaidi ya wanaharakati 600 wa Qur’ani kutoka vituo vya kitamaduni na kisanaa vya misikiti ya Iran.
Shindano lilihitimishwa Ijumaa katika hafla maalumu mjini Hamedan.
Ujumbe wa Rais Pezeshkian ulisomeka kama ifuatavyo:
“Kufanyika kwa mashindano ya Qur’ani ya ‘Mudha Mattan’ ni kuheshimu na kuinua hadhi ya utamaduni wa Qur’ani na wanaharakati wa Qur’ani katika ardhi hii ya elimu na maarifa. Qur’ani Tukufu, kama Kitabu cha milele cha uongofu na muujiza wa Wahyi, ni taa angavu inayoongoza maisha ya binafsi na ya kijamii; na kusoma, kutafakari, na kutenda kwa mujibu wa mafundisho yake ni njia tukufu kabisa ya kujenga roho na maadili ya kizazi kipya.
Kama tunavyosoma katika Qur’ani: *“Hakika hii Qur’ani inaongoa kwenye yaliyo nyooka kabisa.”* Hivyo basi, lengo kuu la mashindano kama haya ni kupata maadili na thamani za kiroho zinazotokana na Kitabu hiki Kitukufu.
Duru ya 17 ya mashindano haya, ambayo mwaka huu yanafanyika chini ya anuani angavu ya “Tamasha la Aya”, Hamedan na kujikita katika misikiti na mitaa, ni ishara ya mwamko wa wananchi katika kueneza utamaduni wa Qur’ani na kuimarisha roho ya kiroho katika jamii. Jukumu la vituo vya misikiti katika kulea na kuandaa vijana waaminifu na wenye juhudi katika uwanja huu wa ujenzi wa fikra ni jambo la kupongezwa mno.
Ubunifu mpya wa mashindano haya ya kikundi umeweka msingi wa kuimarisha ushirikiano, huruma, na kukuza stadi za kufanya kazi kwa pamoja miongoni mwa washiriki. Haya ni majaribio ya aina yake katika elimu na mashindano ya Qur’ani, yanayochanganya elimu ya Qur’ani na kazi za pamoja, pamoja na kukuza hisia ya uwajibikaji na ushiriki wa pamoja kwa vijana, hasa katika mazingira ya mitaa.
Tunatarajia kuwa mwamko huu wenye thamani na baraka utaathiri mipango ya baadaye ya vituo vya Qur’ani, na kufungua njia ya kuendeleza utamaduni wa Qur’ani katika mitaa na jamii nzima, na hivyo kukuza zaidi maendeleo ya kiroho na maadili ya vijana wetu.
Tunaamini kuwa jamii yenye uhusiano wa kina na Qur’ani ni jamii imara, yenye afya, yenye uadilifu na matumaini. Katika uwanja wa utamaduni wa kijumla, iwapo tunatafuta amani katika familia, uaminifu na huruma katika jamii, na iwapo tunataka vijana wetu wapenzi wajenge mustakabali kwa matumaini na uimara, basi njia ni kurejea katika mafundisho ya Qur’ani na kuhuisha roho yake katika tabia, maamuzi na maisha ya kijamii.
Mwisho, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wote waliotekeleza jukumu la kuandaa tukio hili lenye thamani, ambao kwa juhudi zao za ikhlasi wameutia harufu nzuri ya aya za Qur’ani anga ya jamii yetu, na kuwapatia vijana wetu sababu ya matumaini, furaha, na hamasa ya Qur’ani. Namwomba Allah Mtukufu atujalie taufiki ya kutenda kwa mujibu wa Qur’ani na kueneza maadili yake.”
3495395