IQNA

Dunia yakemea shambulio la Waisraeli dhidi ya msikiti wa Palestina

11:34 - November 15, 2025
Habari ID: 3481520
IQNA – Shambulio lililofanywa na kundi la walowezi haramu wa Kizayuni dhidi ya msikiti katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel Ukingo wa Magharibi limeibua ghadhabu na ukemeaji kutoka pande mbalimbali duniani.

Tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari  Israel dhidi ya Gaza, kumeshuhudiwa ukatili wa walowezi hao, uvamizi wa kijeshi unaofwanya na Israel, na kufurushwa kwa nguvu kwa Wapalestina vikizidi

Walowezi hao wa Kizayuni waliteketeza moto Msikiti wa Hajja Hamida ulioko kijiji cha Deir Istiya, kaskazini-magharibi mwa mji wa Salfit, alfajiri ya Alhamisi.

Picha zilizopigwa katika eneo la tukio zilionyesha maandishi ya kibaguzi dhidi ya Waarabu na Waislamu yakiwa yamechorwa kwenye kuta za msikiti, ambao uliharibiwa vibaya na moto huo. Nakala za Qur’ani Tukufu pia ziliteketezwa.

Shirika rasmi la habari la Palestina WAFA, likimnukuu mwanaharakati wa kupinga upanuzi wa makazi Nazmi Salman, liliripoti kuwa wakazi wa eneo hilo waliingilia kati kuzuia moto usienee ndani ya msikiti mzima.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema taasisi hiyo ya kimataifa “inakemea vikali” shambulio hilo.

“Maeneo ya ibada lazima yaheshimiwe na kulindwa kila wakati,” alisema Stephane Dujarric akiwaeleza waandishi wa habari katika makao makuu ya UN mjini New York.

Alilaani “mashambulio yote ya walowezi Waisraeli dhidi ya Wapalestina na mali zao katika Ukingo wa Magharibi.” Akaongeza: “Matukio haya ni sehemu ya muundo unaoongezeka wa ukatili wa misimamo mikali unaochochea mvutano na lazima yakome mara moja.”

Dujarric pia alisisitiza kuwa “Israel, kama nguvu inayokalia kwa mabavu, ina wajibu wa kuwalinda raia wa Palestina na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa.”

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Ukombozi wa Palestina, Hamas, ililaani shambulio hilo la moto kama “uhalifu wa kikatili na dhihirisho la dharau kubwa kwa hisia za Waislamu na uhuru wa ibada.” Ikasema kuwa tukio hilo “limefichua tena kiwango cha ukatili na ubaguzi unaotekelezwa na uvamizi dhidi ya watu wetu na maeneo yetu matakatifu ya Kiislamu na Kikristo.”

Jordan kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Wakimbizi pia ilikemea vikali mashambulio ya walowezi wa Kiyahudi. Msemaji wa wizara hiyo, Fouad Majali, alisisitiza msimamo wa Amman wa kukataa mashambulio hayo, akiyataja kama “mwendelezo wa sera za misimamo mikali za utawala wa Israel na kauli za maafisa wake zinazochochea chuki na ukatili dhidi ya watu wa Palestina.”

Majali alionya kuwa ukiukaji unaoendelea katika Ukingo wa Magharibi na vizuizi vinavyowekwa kwa Wapalestina, vikichanganyika na mashambulio ya walowezi, vinatishia kuibua machafuko zaidi na kuhatarisha usalama wa eneo lote.

Alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kutekeleza wajibu wake wa kisheria na kimaadili, na kuilazimisha Israel kusitisha uchokozi wake hatari na mashambulio ya walowezi, na kutimiza haki halali za Wapalestina za kuanzisha dola huru na yenye mamlaka kamili katika mipaka ya Juni 4, 1967, ikiwa na Quds Mashariki kama mji mkuu wake.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi pia ilieleza wasiwasi mkubwa juu ya ongezeko la ukatili wa walowezi wa Kiyahudi dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.

“Ukatili huu na upanuzi unaoendelea wa makazi haramu lazima ukome,” ilisema taarifa hiyo.

Ujerumani pia ilitoa wito wa kusitishwa kwa mashambulio ya walowezi, ikisisitiza kuwa “matukio haya lazima yachunguzwe kwa kina na wahusika wawajibishwe.”

Mnamo Julai 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilitangaza kuwa uvamizi wa Israel wa Palestina ya kihistoria kwa miongo kadhaa ni haramu. Mahakama hiyo ilitaka kuondolewa kwa makazi yote yaliyopo katika Ukingo wa Magharibi na Quds Mashariki. Ingawa maoni hayo ya ushauri si ya kisheria moja kwa moja, yana uzito mkubwa kisiasa kwani ni mara ya kwanza ICJ imetoa msimamo kuhusu uhalali wa uvamizi wa miaka 57.

3495391

captcha