IQNA

Mwanazuoni: Qur’ani Tukufu Ni Ramani ya Maisha Mema

20:14 - November 14, 2025
Habari ID: 3481515
IQNA – Qur’an Tukufu ni ramani ya kuishi maisha mema, amesema mwanazuoni wa Kiislamu nchini Iran, akiongeza kuwa wale wanaoshikamana zaidi na Qur’ani huishi maisha ya heri na ya uadilifu yanayopendeza kwa Mwenyezi Mungu.

Hujjatul Islam Abbas Mohammad Hassani, Mkuu wa Idara ya Kiitikadi na Kisiasa ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Ian, alitoa kauli hiyo Jumatano alipotembelea Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Jeshi, ambapo maandalizi yanaendelea kwa Mashindano ya 25 ya Qur’ani kwa wanawake wa jeshi na familia zao.

Alisema: “Qur’ani ni kitabu kitakatifu cha Waislamu na ramani ya maisha mema. Kwa hivyo, wale wanaoishi maisha ya Qur’ani wanaishi maisha ya heri yanayokubalika na kupendeza kwa Mola Mtukufu.”

Kwa furaha, aliongeza kuwa Jeshi, lenye historia ya miaka 45 ya shughuli za Qur’ani, limeweza kupata mafanikio mengi katika kuwaleta karibu askari na familia zao na Neno la Wahyi.

Alibainisha kuwa shughuli za Qur’ani katika Jeshi zilianza miaka miwili baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na tangu wakati huo Jeshi limeingia katika nyanja mbalimbali za Qur’ani na kufanikisha mafanikio makubwa.

“Tumejishughulisha katika nyanja zote za Qur’ani, ikiwemo kuhifadhi, kusoma kwa sauti, na kuelewa maana. Bila shaka haya yote ni utangulizi wa kuishi kwa mujibu wa Qur’ani. Ikiwa tunahifadhi lakini hatuishi kwa mafundisho yake, hasara ni kubwa zaidi, kwa kuwa mhifadhi wa Qur’ani anatarajiwa kuwa mjumbe wa Neno Tukufu la Allah.”

Akirejelea mashindano yajayo, alisema: “Hakuna kitu kinachoitwa kushindwa katika mashindano ya Qur’ani. Yeyote anayeshiriki katika programu za Qur’ani ni mshindi. Ni lazima ieleweke kuwa kadri tunavyopiga hatua zaidi katika uwanja wa Qur’ani, ndivyo tunavyopata mafanikio ya kiroho na baraka nyingi zaidi.”

3495387

captcha