IQNA

Waislamu wa Uingereza wamuomboleza Askofu Tutu

16:45 - December 27, 2021
Habari ID: 3474729
TEHRAN (IQNA)- Baraza la Waislamu Uingereza limetuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini.

Askofu Mkuu mstaafu Desmond Tutu, ambaye ni nembo ya harakati za kupiga vita mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apathaidi nchini Afrika Kusini alifarikia Dunia Disemba 26 akiwa anapata matibabau nchini Afrika Kusini.

Ujumbe wa Baraza la Waislamu Uingereza ulimtembelea Askofu Tutu mwaka 2009 kujadili njia za kuleta pamoja jamii mbali mbali. Askofu Tutu alikuwa mstari wa mbele kuwatetea wananchi wa Palestina wanaodhulumiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Uingereza Zara Mohammad amesema: "Aksofu Desmond Tutu alikuwa kiongozi mwenye mfano wa kuigwa katika zama zetu. Alisimama katika imani yake na kutetea haki bila kuogopa huku akipambana na dhulma na alijitahidi kupatanisha kila alipoweza."

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Askofu Desmond Tutu, aliyeipigania Afrika Kusini akiwa na hayati Nelson Mandela, rais wa kwanza mweusi katika taifa hilo, alikuwa akilazwa mara kwa mara hospitalini.

Kiongozi huyo wa kidini aliongoza maandamano na kampeni nyingi kwa lengo la kutokomeza mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na anajulikana pia kama nembo kubwa ya utetezi wa demokrasia nchini humo.

Yeye ni rafiki wa muda mrefu pia wa Mzee Mandela, ambaye naye pia alishinda tuzo ya amani ya Nobeli, na wawili hao wamewahi pia kukaa mtaa mmoja wa Vilakazi katika mji wa Soweto, ambao ni mtaa pekee duniani kutoa washindi wawili wa tuzo hiyo ya kimataifa inayoheshimika.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amemlilia Askofu Tutu akisema, huo ni msiba mwingine mkubwa kwa nchi hiyo, kutokana na Mwafrika Kusini mwingine mashuhuri kuondoka katika sura ya dunia.

Ramaphosa amesema, kiongozi huyo wa kidini alikuwa mtu mashuhuri ndani na nje ya Afrika Kusini na akaongeza kwamba "kwetu sisi ametuachia urithi mkubwa utakaodumu vizazi hadi vizazi."

4023817/

captcha