IQNA

Imam Khamenei asisitiza kusimama kidete taifa la Iran

11:36 - November 23, 2013
Habari ID: 1321100
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha sifa na hila za kidanganyifu na kutokubali haki ubeberu wa dunia unaoongozwa na Marekani na kuongeza kuwa, njia pekee ya kuweza kumkatisha tamaa adui ni kusimama kidete na kuimarisha nguvu za taifa. Aliyasema hayo Jumatano asubuhi aliponana na makumi ya maelfu ya makamanda wa jeshi la Basiji na kusema kuwa, Basiji ni moja ya madhihirisho ya uthabiti, fakhari na utukufu wa mfumo wa utawala wa Kiislamu.


Vile vile amesisitiza kuwa, anaiunga mkono kikamilifu Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jitihada zinazofanywa na viongozi nchini na kuongeza kuwa, mistari myekundi ni lazima ilindwe katika kadhia ya nyuklia na wanaoendesha mazungumzo ya nyuklia hawapaswi kurudi nyuma hata kwa hatua moja katika kutetea haki za taifa la Iran.

Aidha katika mjumuiko huo mkubwa, Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja jeshi la Basiji kuwa ni dhihirisho la utukufu wa taifa la Iran na ni nguvu yenye umuhimu mkubwa ya ndani ya nchi na kusisitiza kuwa, jeshi la Basiji linawafurahisha marafiki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuwapa moyo na matumaini kama ambavyo jeshi hilo linawatia khofu na kuwaogopesha mno maadui wenye chuki na wanaoutakia mabaya mfumo wa utawala wa Kiislamu.

Pia ameashiria namna Wiki ya Basiji nchini Iran ilivyosadifiana na hamasa kubwa za Bibi Zaynabul Kubra Salamullahi Alayha na kuongeza kuwa, hamasa ya Bibi Zaynab ilikuja kukamilisha hamasa ya ‘Ashura. Aidha amesisitiza kusisitiza kuwa, utukufu wa kazi iliyofanywa na Bibi Zaynab Salamullahi Alayha inaweza kutathminiwa na kufananishwa na hamasa ya ‘Ashura tu na kwa maneno mengine ni kuwa hamasa ya Bibi Zaynab Salamullahi Alayha ulikuwa ni muendelezo na ilikuwa ni katika kuilinda hamasa ya 'Ashura.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, Bibi Zaynab Salamullahi Alayha ambaye ni Bibi mtukufu katika Uislamu na ubinadamu alisimama imara mithili ya jabali lenye vilele virefu na lisilotetereka mbele ya masaibu na matukio machungu yaliyomkumba na kufanikiwa kuwa kigezo na ruwaza njema iliyodumu milele.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia hotuba iliyoonesha msimamo usiotetereka na wakati huo huo iliyokuwa wazi na iliyojaa balagha iliyotolewa na Bibi Zaynabul Kubra Salamullahi Alayha mbele ya watu wa Kufa na vile vile mbele ya Yazid na kusisitiza kuwa: Bibi huyo mtukufu alikuwa ni dhihirisho la heshima kama alivyokuwa Imam Husain Alayhis Salaam, siku ya ‘Ashura.

Amesema, matunda ya kusimama kidete Bibi Zaynab Salamullahi Alayha ni kuzuka harakati katika zama zote ambayo inachukua ilhamu ya kusimama kidete kwenye njia ya haki kutoka katika hamasa ya mtukufu huyo.

Ameongeza kuwa, inabidi kigezo cha harakati yetu na misimamo yetu siku zote iwe ni hamasa ya Bibi Zaynab Salamullahi Alayha na lengo letu liwe ni kuuletea heshimu Uislamu na jamii ya Kiislamu pamoja na kupigania heshima ya mwanadamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja sababu kuu iliyopelekea kushuhudiwa moyo wa namna hiyo wa Bibi Zaynab Salamullahi Alayha na mawalii, Mitume na waumini kwamba ni kuwa na yakini na ahadi ya Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Qur'ani Tukufu inasema kwamba kuwa na yakini hiyo ni wajibu kwa Mitume na Manabii watukufu wa Mwenyezi Mungu na mawalii na watu wa kawaida na kwamba sisi sote tuna wajibu wa kutekeleza vilivyo majukumu yetu kuhusu ahadi tuliyoitoa kwa Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Udhmna Khamenei amesisitiza pia kuwa, kwa mujibu wa ‘nasi' iliyo wazi ya Qur'ani Tukufu, ahadi hiyo ni kusimama imara katika kukabiliana na adui kwenye mapambano ya kijeshi, ya kisiasa na ya kiuchumi na kutogeuka nyuma kumkimbia adui.

Amesema, kwa mujibu wa ahadi hiyo, sehemu yoyote ile palipo na mapambano inabidi kuwe na kusimama imara kukabiliana na adui na inabidi azma na ari ya Waislamu na waumini siku zote iishinde azma na nia ya adui.

Katika sehemu hiyo ya miongozo yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria istilahi ya "ulaini wa kishujaa" aliyoitumia hivi karibuni na kuongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu wameifasiri istilahi ya ulaini kwa kishujaa kuwa ni kuachama na usuli na malengo matukufu ya mfumo wa utawala wa Kiislamu na baadhi ya maadui nao wametumia jambo hilo kudai kuwa Jamhuri ya Kiislamu imeachana na misingi yake mikuu lakini ukweli wa mambo ni kuwa wamefahamu vibaya na wameelewa kinyume na uhalisia wa mambo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Istilahi ya "ulaini wa kiushujaa" ina maana ya kufanya manuva kwa usanii wa hali ya juu na kutumia mbinu za kila namna kwa ajili ya kufikia shabaha na malengo matukufu tofauti ya Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia malengo tofauti ya mfumo wa Kiislamu wa utawala, kwa ajili ya maendeleo na kuleta ustaarabu adhimu wa Kiislamu na kuongeza kuwa, malengo hayo yanafuatiliwa kwa sura ya hatua kwa hatua na kipande kimoja baada ya kingine ambapo watu wanaotoa miongozo, waongozaji na wanafikra wanayawekea awamu zake maalumu malengo hayo na baadaye ndipo huanza harakati kuu ya wote.

Vile vile amesema: Huu, ni mfumo sahihi wa harakati ya kimantiki ya kuiletea maendeleo Jamhuri ya Kiislamu mfumo ambao watu wote wanaofanya katika katika masuala ya kisiasa na viongozi wakuu wa nchi pamoja na waamilifu na wanaharakati katika uwanja wa Basiji wanapaswa kuuzingatia.

Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza maswali kadhaa akisema: Je wakati mfumo wa utawala wa Kiislamu unaposisitiza juu ya suala la maendeleo una maana ya kupenda vita? Je, Jamhuri ya Kiislamu inapenda kuwa na mikwaruzano na mataifa na tawala zote duniani? Lakini hayo yanasemwa baadhi ya wakati na ndimi za baadhi ya maadui wa taifa la Iran zikiwemo ndimi najisi zilizojaa nuhsi za mbwa kichaa wa eneo la Mashariki ya Kati yaani utawala wa Kizayuni.

Ayatullah Udhma Khamenei amesema, madai hayo ya adui yanakinzana kikamilifu na mtazamo na mwenendo wa Uislamu, wakati lengo la Jamhuri ya Kiislamu linafuatiliwa kwa mujibu wa somo linalotolewa na Uislamu na Qur'ani Tukufu na Mtume Muhammad SAW na Maimamu watoharifu Alayhimus Salaam yaani malengo ya kusimamisha uadilifu, ihsani na matendo mema kwa mataifa yote.

Amesisitiza kuwa, kitisho hasa kinachohatarisha usalama duniani ni kuweko nguvu inayopenda shari ukiwemo utawala pandikizi wa Kizayuni na waungaji mkono wake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu siku zote imekuwa ikipigania kuweko mapenzi na kuwahudumia watu wote na kuwa na uhusiano wa kirafiki na mataifa yote duniani.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haina uadui wowote na mataifa ya dunia na hata na wananchi wa Marekani ijapokuwa watawala wa Marekani ni mabeberu, ni maadui na wana chuki, wanafanya uhasama wa kila namna na wanalitakia mabaya taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu.

Amesisitiza kuwa, kitu ambacho kinakabiliana na Jamhuri ya Kiislamu na ambacho mfumo wa utawala wa Kiislamu nao unapambana nacho, ni uistikbari na ubeberu wa kimataifa.

Baada ya kusisitizia uhakika huo, Ayatullah Udhma Khamenei ameendeleza hotuba yake mbele ya makumi ya maelfu ya makamanda wa jeshi la Basiji kwa kubainisha sifa kadhaa za kihistoria na mifano yake katika zama za hivi sasa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja neno uistikbari kuwa ni istilahi iliyomo kwenye Qur'ani Tukufu na kuongeza kuwa, skeletani ya uistikbari na ubeberu imekuwepo katika kipindi chote cha historia ingawa mbinu na njia zake zimekuwa zikitofautiana.

Aidha amesisitiza kuwa yeye anapinga kuchukuliwa hatua zozote zisizo za kimantiki na zisizo za busara katika jambo lolote lile na kuongeza kuwa, inabidi hekima itumike, busara, umakini na tadibiri itumike katika mambo yote ikiwa ni pamoja na katika medani za kupambana na kukabiliana na uistikbari.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamku ametaja mambo ya dharura ya kuweza kukabiliana kwa njia za busara na hekima na uistikbari kuwa ni kutambua sifa na dhati ya miamala, mikakati na misimamo ya mfumo wa kibeberu na kuongeza kwamba, ni jambo lisiloyumkinika kuweka mikakati na mipango ya kukabiliana kwa busara na kwa hekima na mfumo wa kibeberu bila ya kuwa na utambuzi wa kutosha na sahihi kuhusu mfumo huo.

Vile vile amebainisha sifa za miamala ya mfumo wa kiistikbari kwa kutaja moja ya sifa kuu za mfumo huo wa kibeberu yaani namna mabeberu wanavyojiona bora kuliko watu wengine wote.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, wakati nchi fulani inapojiona bora na kujifanya ndio mhimili na marejeo makuu ya mfumo wa kimataifa, hupelekea kushuhudiwa hali ya hatari na ya kutisha katika miamala ya kimataifa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kujipa haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyinginezo, kuyabebesha mataifa mengine mambo yanayotakiwa na taifa fulani tu na taifa hilo kudai kuwa ndilo linaloongoza masuala ya dunia ni miongoni mwa matokeo mabaya na ya hatari ya kujiona bora mfumo wa kibeberu dhidi ya mataifa mengine.

Ameongeza kuwa, viongozi wa Marekani wanazungumza kwa sura ambayo utadhani wao ndio wanaoyamiliki mataifa yote ya dunia na wao ndio wanaoimiliki ulimwengu na eneo letu hili.

Ayatullah Udhma Khamenei ametaja hatari nyingine kuwa ni kutokubali haki mataifa yanayojiona bora kuliko mataifa mengine yaani madola ya kibeberu.

Vile vile ameashiria jinsi mabeberu na viongozi wa Marekani wanavyoshikilia misimamo yao na kutokubali kutambua haki za mataifa mengine duniani ameongeza kuwa: Kadhia ya nyuklia ya Iran ni mfano wa wazi wa jinsi mabeberu wanavyosimama imara kupinga haki ya taifa la Iran katika suala hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mtu au nchi yoyote ile inapokuwa na busara na mantiki huukubali mara moja ukweli unapothibitishwa mbele yake lakini mabeberu hawatambui maneno ya haki na wala hawako tayari kuikubali haki iliyo wazi ya watu wengine bali hata wanafanya njama za kukanyaga haki za watu hao.

Ayatullah Udhma Khamenei amesema, suala la kuona ni halali kutenda jinai dhidi ya mataifa mengine, ni sifa nyingine mbaya na madola ya kibeberu na kuongeza kuwa: Mabeberu hawawathamini wala kuwapa thamani yoyote watu wanaowapinga na wasiokubali kufuata siasa zao na wanahalalisha kutenda jinai yoyote ile dhidi yao.

Vile vile ametoa ufafanuzi kuhusu mifano mbali mbali isiyo na mwisho katika uwanja huo na kutaja vitendo vya kuchefua moyo vilivyofanywa na mabeberu dhidi ya wenyeji wa bara la Amerika, jinai zilizofanywa na Waingereza dhidi ya wenyeji wa Australia na namna Waafrika walivyofanywa watumwa na Wazungu na kupelekwa katika bara la Amerika.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekitaja kitendo cha Wamarekani kutumia bomu la atomiki huko nchini Japan kuwa ni mfano mwingine wa jinai za zama hizi zilizofanywa mabeberu na kufafanua kwa kusema: Duniani kumewahi kutumika mara mbili tu bomu la atomiki na mara zote mbili bomu hilo limetumiwa na Wamarekani dhidi ya watu wa Japan. Hata hivyo na licha ya Wamarekani kufanya jinai hiyo lakini leo hii Marekani inajifanya kuwa ndiye msimamiaji wa suala la nyuklia ulimwenguni.

Kiongozi Muadhamu wa Mapionduzi ya Kiislamu amekumbushia pia namna Wamarekani walivyofanya mauaji ya kutisha na mateso makali dhidi ya wananchi wa Vietnamn, Iraq, Pakistan na Afghanistan na kuongeza kuwa, kamwe walimwengu hawawezi kusahau mateso ya kiuadui na ya chuki wanayofanyiwa watu katika jela za Guantano na yaliyofanywa kwenye jela ya Abu Ghuraib huko Iraq.

Akiendelea kutoa ufafanuzi kuhusu udharura wa kutambua sifa za mabeberu kwa ajili ya kukabiliana na mfumo wa kiistikbari kwa kutumia hekima, tadibiri na busara, Ayatullah Udhma Khamenei amegusia sifa nyingine waliyo nayo mabeberu nayo ni unafiki na udanganyifu.

Amefafanua suala hilo kwa kusema: Miongoni mwa mbinu na hila zinazotumiwa sana na mabeberu ni kuzivika jinai zao nguo ya kutoa huduma kwa watu na kuutumikia ubinaadamu.

Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna propaganda za Wamarekani zinavyofanya kazi ya kuhalalisha mashambulizi ya atomiki yaliyofanywa na Marekani nchini Japan na kuongeza kuwa, Wamarekani wanadai kuwa lau kama watu laki mbili wasingeliuliwa kwa umati kwa kutumia mabomu ya atomiki kwenye miji ya Nagasaki na Hiroshima huko Japan, basi Vita vya Pili vya Dunia visingelimalizika, bali jamii ya mwanadamu ingelilazimika kupoteza watu milioni mbili hivyo kwa hakika hatua ya Wamarekani ya kushambulia kwa mabomu ya atomiki miji hiyo ya Japan ilikuwa ni kwa faida dunia nzima na ilikuwa ni kwa ajili ya kuitumikia jamii nzima ya mwanadamu.

Ameongeza kuwa, uongo huo unaoenezwa na Wamarekani ni udanganyifu mkubwa ambao unakaririwa mara kwa mara na sababu ya kusema kuwa ni uongo ulio dhahiri ni kuwa kwa mujibu wa ushahidi uliopo, miezi kadhaa kabla ya Wamarekani kutenda jinai kubwa ya kuwaua kwa halaiki wananchi wa Japan kwa kutumia mabomu ya atomiki, Hitler ambaye alikuwa sababu kuu ya Vita vya Pili vya Dunia, alikuwa ameshajiua zamani.

Mussolini, yaani nguzo nyingine ya Vita vya Pili vya Dunia alikuwa ameshatiwa mbaroni kabla ya mashambulizi hayo ya mabomu ya atomiki ya Marekani huko Japan na hata viongozi wenyewe wa Japan walikuwa wameshatangaza kuwa wako tayari kusalimu amri miezi miwili kabla ya mashambulio hayo ya mabomu ya atomiki ya Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi kuhusu sababu hasa iliyowafanya viongozi wa Marekani washambulie kwa atomiki miji ya Nagasaki na Hiroshima ya Japan kwa kusema kwamba, ukweli ni kuwa Wamarekani walitaka kujaribisha silaha yao mpya yaani bomu la atomiki katika medani ya kweli ya vita shambulio ambalo lilipekekea kuuawa kwa umati na kwa mkupuo mmoja makumi ya maelfu ya wananchi wasio na hatia wa Japan na athariu zake mbaya zinaendelea hadi hivi sasa lakini leo hii Wamarekani wanafanya propaganda kubwa ya kuzivika jinai zao hizo, guo la kuhudumia ubinadamu na walimwengu.

Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mfano mwingine wa unafiki na uongo wa mfumo wa kibeberu kwa kuashiria kadhia ya kutumiwa silaha za kemikali nchini Syria.

Amesema kuwa, Rais wa Marekani na viongozi wa nchi hiyo wanadai kwamba kutumia silaha za kemikali ni msitari mwekundu, lakini watawala hao hao wa Marekani, wakati utawala wa Saddam ulipotumia silaha za kemikali dhidi ya wananchi wa Iran si tu hawakupinga jinai hiyo, bali walifikia hadi ya kuupatia utawala wa Saddam tani zisizopungua mia tano za mada hatari mno za kemikali ambapo dikteta huyo wa Baghdad alizitumia kutengenezea gesi hatari mno ya kemikali na kuitumia dhidi ya wanapambano waliokuwa wakilinda nchi yao wa Iran.

Vile vile ameashiria kuuawa karibu wasafiri 300 kutokana na shambulio lililofanywa na meli ya kivita ya Marekani dhidi ya ndege ya abiria ya Iran na jinsi Wamarekani walivyokuwa wakimsaidia kwa taarifa mbali mbali za kijasusi Saddam bila ya wasiwasi wowote na kusema kuwa hiyo ni mifano mingine ya jinai za utawala wa kibeberu wa Marekani na kuongeza kuwa: Kufanya uvamizi na kuendesha vita pamoja na kueneza fitna na mifarakano ni sifa nyingine mbaya za mfumo wa kibeberu.

Katika sehemu nyingine ya miongozo yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna kambi ya haki inavyopambana na kambi ya kibeberu na kiistikbari katika kipindi chote cha historia na kuuliza swali hili la kimsingi kwamba ni ipi hasa sababu inayoifanya kambi ya kibeberu kukabiliana na kufanya njama za kila namna dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu?

Akijibu swali hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ushahidi kuhusu sababu kuu iliyopelekea kutokea Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kuongeza kuwa: Mapinduzi ya taifa kubwa la Iran na mfumo wa utawala uliochaguliwa na taifa hili, kimsingi umetokana na taifa la Iran kupinga ubeberu na vitu vinavyotia nguvu uistikbari. Mfumo wa utawala wa Kiislamu nao umenawiri na kuimarika kwa fikra hiyo na ndio maana kwa kuona sifa hizo za Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa utawala wa Kiislamu nchini Iran, mabeberu wakashindwa kabisa kuuvumilia mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na wataendelea vivyo hivyo ila pale watakapokatishwa tamaa kikamilifu katika njama zao za kutaka kuuvunja na kuushinda mfumo huo.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria udharura wa kuhakikisha kuwa adui anakatishwa tamaa kikamilifu suala ambalo amesema ni la msingi kabisa katika kuzuia uadui wa mabeberu na njama zao dhidi ya taifa la Iran na kusisitiza kuwa: Matabaka mbali mbali ya wananchi na watu wote ambao kwa namna moja au nyingine na hata kwa sababu isiyokuwa ya Kiislamu, wana uchungu na nchi na ardhi yao wanapaswa kuhakika kuwa nyoyo za adui zinakatishwa tamaa ili kwa njia hiyo maadui hao wavunjike moyo kikamilifu katika njama zao zote.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kuendelea kuwepo uadui wa wakati wote wa Marekani tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu hadi leo hii na kuongeza kuwa, kufanya uchochezi kati ya makabila, kufanya mapinduzi ya kijeshi, kumchoche Saddam na kumpa misaada ya kila namna ili avamie Iran na kuendesha vita vya miaka minane na kuliwekea mashinikizo ya kila namna taifa Iran yote hayo ni miongoni mwa mifano ya kuwepo uadui usiokoma na usio na mwisho wa Marekani dhidi ya taifa hili ambalo miaka thelithini na tano iliyopita lilianzisha harakati huru ya kujitegemea katika eneo muhimu na nyeti sana la magharibi mwa bara la Asia na licha ya kuwepo uadui wote huo dhidi yake, lakini taifa la Iran limestawi na limegeuka kuwa kugezo kizuri kwa mataifa mengine ya eneo hili.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna rais wa hivi sasa wa Marekani alivyohusika katika njama za fitna ya mwaka 2009 nchini Iran na kuongeza kuwa: Katika mwaka huo kulikuwa na mtandao moja wa kijamii ambao ulihitajia matengenezo, lakini rais wa Marekani alizuia kufanyika matengenezo hayo ili kutoa fursa kwa mtandao huo wa kijamii kusaidia kueneza moto wa fitna nchini Iran.

Ameongeza kuwa: Wamarekani walikumbwa na ndoto za mchana na za kipumbavu kwamba mitandao ya kijamii kama vile Twitter na Facebook ingeliweza kuupindua mfumo wa utawala wa Kiislamu nchini Iran na ndio maana walitumia mbinu zao zao kujaribu kufanikisha njama zao kupitia mitandao hiyo, (lakini walishindwa).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amevitaja vikwazo kuwa ni moja ya njia na mbinu zinazotumiwa na adui kujaribu kulishinda taifa la Iran na kusisitiza kuwa, tatizo la maadui ni kwamba, wanashindwa kulitambua taifa la Iran pamoja na itikadi, imani na mshikamano wake na wanashindwa kupata funzo kutoka katika makosa yao na kufeli mara kwa mara katika njama zao.

Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi kutoka katika msimamo ambao daima unatangazwa na taifa la Iran na mfumo wa utawala wa Kiislamu nchini katika kipindi chote hiki cha miaka 35 iliyopita na kuongeza kuwa: mafanikio yote liliyoyapata taifa la Iran sambamba na kushindwa mara kwa mara mabeberu wa dunia yanatokana na jambo hilo na ni jambo linalothibitisha kwamba, kuwa na nguvu na kusimama imara ndiyo njia pekee ya kuweza kupambana na kuyashinda maudhi na usumbufu wa adui na kumlazimisha arudi nyuma na kwamba taifa la Iran linalitambua vyema jambo hilo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia kadhia ya mazungumzo ya nyuklia na mijadala inayohusiana na suala hilo na kusema kuwa: Mimi ninaiunga mkono Seerikali na viongozi wetu wa humu ndani na viongozi wetu waliopewa jukumu la kuendesha mazungumzo hayo na ninalisisitizia sana suala hilo kwani ni jukumu langu kuziunga mkono serikali zote zinazoingia madarakani humu nchini.

Ameongeza kuwa: Mimi nilikuwa na jukumu la kuendesha serikali kwa miaka mingi na ninajua vizuri uzito na tabu za kazi ya kuendesha mambo ya utekelezaji ya nchi na ninatambua vyema kuwa viongozi serikalini wanahitaja uungaji mkono na kusaidiwa, hivyo uungaji mkono wangu kwa serikali na viongozi wetu ni jambo ambalo ninalifanya kwa udhati wa moyo wangu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Tab'an katika upande mwingine, ninasisitizia sana wajibu wa kulindwa haki za taifa la Iran ikiwa ni pamoja na haki za nyuklia na ninasisitiza mno kuwa haipasi kurudi nyuma hata kwa hatua moja katika suala la kulinda na kuteteaa haki za taifa la Iran.

Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Mimi siingilii vipengee vidogo vidogo vya mazungumzo hayo lakini kuna mistari myekundu ambayo inabidi isivuukwe na viongozi husika nao wana jukumu la kuchunga mistari hiyo isivuukwe na wala hawapaswi kujitia woga kutokana na propaganda na vitisho vya adui.

Amesema kuwa, sababu kuu ya vikwazo linavyowekewa taifa la Iran ni chuki za dola la kibeberu la Marekani. Ameongeza kuwa, Marekani inalifanyia uadui wa kila namna taifa la Iran na kwamba lengo la maadui la kuliwekea vikwazo taifa hili ni dhana potofu ya madola hayo yanayoota kuwa labda kuna siku taifa la Iran litasalimu amri, lakini wanajidaganya kwani vikwazo haviwezi kulifanya taifa la Iran lisalimu amri kwa mtu yeyote yule.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema: Kwa taufiki na msaada wa Mwenyezi Mungu, taifa la Iran litavistahamilia vikwazo hivyo na kuvigeuza kuwa fursa za kuzidi kujiimarisha na kujiletea maendeleo.

Ayatullah Udhma Khamenei aidha ameashiria baadhi ya nukta dhaifu katika kuchukua maamuzi na kuweka mipango ya kiuchumi nchini na ndoto ya adui ya kujipenyeza na kutumia vibaya nukta hizo akisema kwamba: Tofauti na anavyoota adui, mashinikizo hayo yatakuwa fursa nzuri ya kutuwezesha kuondoa nukta zetu dhaifu.

Amesisitiza kwamba, vikwazo na mashinikizo hayatafaa kitu na hata Wamarekani wenyewe wanalitambua hilo na sababu ya kusema hivyo ni kuwa kila wakati Wamarekani wanapotumia vikwazo, hutoa pia vitisho vya kijeshi na huo ni ushahidi wa wazi kuwa wanajua kwamba vikwazo haviwezi kuwafikisha kwenye malengo yao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amekumbusha kwa kusema: Tab'an hivyo vitisho vya kijeshi ambavyo mara kwa mara utamsikia rais wa Marekani na viongozi wengine wa nchi hiyo wanavitoa dhidi ya taifa la Iran navyo ni kitendo cha kukirihisha kinachochefua moyo.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Rais wa Marekani na viongozi wengine wa nchi hiyo badala ya kutoa vitisho vya kijeshi dhidi ya taifa la Iran wanapaswa kufikiria kwanza njia za kutatua uchumi wao mbovu ulioharibika vibaya na kutafuta njia za kulipa madeni makubwa inayodaiwa Marekani. Wanapaswa waende wakafikirie kwanza njia za kutatua matatizo yao ili kuzuia serikali ya nchi hiyo isilazimike kwenda likizo ya lazima ya wiki mbili nzima.

Amesisitiza kuwa, taifa la Iran linayaheshimu mataifa mengine yote duniani lakini radiamali ya taifa la Iran kwa taifa lolote linalofanya uchokozi dhidi yake yatakuwa ni majibu ya kulitia majuto taifa hilo kwani taifa la Iran litatoa pigo kali kwa mchokozi yeyote yule kiasi kwamba kamwe hataweza kusahau pigo hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja hatua ya viongozi wa Marekani ya kubeba jukumu na kazi ya kutoa matamshi ambayo yanairidhisha kanali ya mabepari wa Kizayuni kuwa ni udhalili, uduni na kukosa kwao hadhi na kuongeza kuwa, hatima ya utawala wa Kizayuni ni kufutika katika uso wa dunia kwani utawala huo pandikizi umeundwa kutokana na kutumia mabavu na kudhulumu watu na kuwabebesha watu hao jambo wasilolitaka na hakuna kitu chochote cha kubebeshwa kinachoweza kudumu.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia kitendo cha kusikitisha na cha aibu cha kutoa matamshi ya kujikomba na kujipendekeza kwa Wazayuni kinachofanywa na baadhi ya tawala za nchi za Ulaya kwa ajili ya Wazayuni ambao hawana ubinadamu wowote na kusema kuwa, kuna wakati taifa la Ufaransa lilipata itibari na heshima ya kisiasa kutokana na rais wa nchi hiyo kusimama na kupinga siasa za Uingereza na Marekani, lakini hivi sasa viongozi wa Ufaransa, si kwamba wanajidhalilisha tu kwa Marekani lakini pia wanajidunisha na kujidhalilisha hata mbele ya utawala najisi na uliojaa nuhsi wa Kizayuni, jambo ambalo kwa kweli ni aibu kwa taifa la Ufaransa na kwamba wananchi wenyewe wa Ufaransa ndio wanaopaswa kuzuia jambo kama hilo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja maana hasa ya Basiji kuwa uwepo na ushiriki wa kweli wa wananchi katika nyuga tofauti na kusisitiza kwamba: Uhakika huu uko wazi na haukanushiki kwamba, wakati wowote wananchi wanapokuwa katika medani, wakashikamana na kuwa kitu kimoja katika medani hiyo, basi bila ya shaka yoyote ushindi unakuwa ni wao.

Vile vile amesema kuwa uwezo wa Basiji unaweza kutatua mambo katika nyuga tofauti na huku akiashiria uwepo wa matabaka mbali mbali ya wananchi na sura kubwa na muhimu za kielimu, kiutamaduni, kisanaa, kisiasa na kijamii katika majimui ya Basij ameongeza kuwa, nguvu na uwezo wa Basiji unapaswa uzidi kuongezwa na kuimarishwa, kadiri inavyowezekana.

Pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kushikamana na mambo muhimu na ya lazima ya kimaadili, kielimu na kijamii kuwa kunaandaa uwanja wa kustawi na kuimarika Basiji na kuongeza kwamba, kutia nguvu subira, kujitolea na unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu, kuongeza uwezo wa ndani ya Basiji, kuwa na malengo, kuwa na mapenzi na watu na kuamiliana kwa njia sahihi na mazingira yalivyo katika jamii pamoja na kufanya idili na jitihada zisizochoka katika kuhudumia watu ni miongoni mwa mambo ya lazima yanayoweza kuisaidia majimui ya Basiji katika kufanikisha malengo ya nchi kadiri siku zinavyosonga mbele.

Katika sehemu ya mwisho ya miongozo yake muhimu sana, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu vijana akiwaambia: Ni jambo lisilo na shaka hata chembe kwamba mustakbali bora na wenye matumaini wa nchi yetu umo mikononi mwenu nyinyi na ni nyinyi vijana ndio mtakaoweza kuifikisha nchi kwenye vilele vya juu vya mafanikio na kuwa kigezo na mfano kamili wa ustaarabu mpya wa Kiislamu.

Ameongeza kuwa, ili vijana waweze kulifanikisha vizuri jukumu hilo wanapaswa kujiimarisha kidini, taqwa, staha na usafi wa roho pamoja na kujiimarisha kielimu, uchapaji kazi, uaminifu, huduma za kijamii na katika sekta ya michezo.

Mwanzoni mwa mkutano huo, na kwa amri ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, awamu ya pili ya luteka na mazoezi ya kijeshi ya brigedi za Basiji imeanza kwa wakati mmoja kwa neno la siri la "Muhammadur Rasulullah" chini ya anwani "Hadi Baytul Muqaddas" katika mikoa 9 ya Iran.

Kabla ya miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Meja Jenerali Muhammadali Jafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, ubeberu wa kimataifa umeanzisha vita vigumu, vipana na vyenye vipengee vingi dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, uimara wa muundo wa ndani ya mfumo wa utawala wa Kiislamu nchini; unahitajia kuimarishwa kila upande Basiji ya wananchi kwa ajili ya kushiriki vilivyo kwenye medani tofauti zinazohitajiwa na Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Meja Jenerali Jafari ameashiria pia namna kulivyowekwa mikakati na misingi mizuri kwa ajili ya Basiji kwa lengo la kufanikisha amri za Amirijeshi MKuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ametaja baadhi ya kazi na hatua zilizochukuliwa ndani ya Basiji kwenye nyuga mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuunda kanali tofauti za watu wema, kanali za kuamrisha mema na kukataza mabaya, ujenzi na ukarabati wa miji na kustawisha maeneo yenye maendeleo duni, kanali za kufanya kazi za ujasiriamali, utafiti wa kielimu, ukuzaji wa vipawa, kazi za watu wenye vipaji maalumu na za matabaka mengine tofauti, kazi zinazohusiana na masuala ya michezo n.k, mambo ambayo ni katika miundombinu ya lazima ya kuweza kutia nguvu uwezo wa Basiji katika kuimarisha nguvu na uimara wa ndani wa mfumo wa Kiislamu wa utawala.

Kwa upande wake Brigedia Jenerali Muhammad Ridha Naqdi, Mkuu wa Taasisi ya Basiji ya Wanyonge nchini Iran ametoa hotuba fupi kabla ya miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiashiria jihadi ya pande zote ya kambi za muqawama ambazo ni uti wa mgongo wa Basiji na kusema: Leo hii kambi za Basiji ni vituo muhimu vya mwamko na ni tegemeo la usalama na amani kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa, hata kama adui atatumia nguvu zake zote za kijeshi, za ubeberu na za udanganyifu za maelfu ya vyombo vyake dhidi ya Iran, kamwe hatutarudi nyuma hata kwa shibri moja katika utiifu wetu wa "Wilaya."

Mwanzoni mwa mkutano pia, baadhi ya mabasiji waliokuwepo kwenye eneo la mkutano walikuwa na ratiba mbali mbali kama ile iliyopewa jina la "Wabeba Bendera ya Ustaarabu wa Kiislamu."



1320240

captcha