Wizara ya Awqaf ya Misri imetangaza kuwa toleo la 33 la tukio hilo la kimataifa la Qur’ani litafanyika mwaka huu likiwa limepewa jina la msomaji maarufu wa Qur’ani katika ulimwengu wa Kiislamu, Sheikh Abdel Fattah Shaasha’i.
Wizara hiyo pia imetangaza tarehe za mitihani ya maandishi kwa hatua ya awali ya mashindano hayo.
Kwa mujibu wa tangazo la wizara, mitihani ya maandishi ya awamu ya awali itaanza Jumatatu tarehe 8 Juni na kuendelea hadi tarehe 18 Juni katika Msikiti wa Nour ulioko eneo la Abbasiya mjini Cairo.
Wizara pia imechapisha majina ya washiriki waliokidhi masharti ya kushiriki katika hatua ya mitihani ya maandishi. Hatua hii inawahusu washiriki waliokamilisha usajili na kukubaliwa kulingana na kanuni na masharti yaliyotangazwa.
Taarifa ya wizara imesisitiza kuwa mashindano hayo yanafanyika kwa lengo la kuwasaidia na kuwahamasisha wahifadhi wa Qur’ani Tukufu, kueneza utamaduni wa Qur’ani, na kuwatia moyo wanaharakati wa Qur’ani kuhifadhi, kutafakari na kuelewa maana za aya za Mwenyezi Mungu.
Wizara imezitaka idara na taasisi zote za mikoa kuwafahamisha watu wanaostahiki kuhusu muda na mahali pa kufanyika kwa mitihani hiyo.
Inafaa kutajwa kuwa matoleo mbalimbali ya Mashindano ya Kimataifa ya Misri ya Kuhifadhi na Kusoma Qur’ani tayari yamewahi kufanyika kwa heshima ya kumbukumbu na majina ya maqari wakubwa wa Misri kama vile Mahmoud Khalil Al‑Husari, Abdul Baset Abdul Samad, na Shahat Muhammad Anwar.
4356312