IQNA

Mashirika 21 ya Huduma za Umrah yafutiwa vibali

15:40 - June 14, 2026
Habari ID: 3482358
IQNA – Katika hatua kali ya kusimamia viwango vya ubora wa huduma, mashirika 21 yanayotoa huduma za Umrah yamesimamishwa kazi kufuatia tathmini ya utendaji iliyofanywa baada ya msimu uliopita.

Wizara ya Hajj na Umrah ya Ufalme wa Saudi Arabia imetangaza kusimamishwa kwa mashirika hayo kutoa huduma za Umrah, baada ya matokeo ya tathmini ya utendaji wa msimu uliopita kubainisha kuporomoka kwa kiwango cha huduma kwa baadhi ya waendeshaji pamoja na ukiukaji wa kanuni zinazosimamia watoa huduma za Umrah.

Uamuzi huu unaakisi maandalizi ya mapema ya wizara kwa ajili ya msimu ujao wa Umrah na dhamira yake ya kuhakikisha waumini wanaotekeleza ibada hii wanapatiwa huduma zilizo bora na zenye kuaminika.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, mashirika 15 yamesimamishwa kutokana na kupata alama za chini katika viashiria vilivyoidhinishwa vya tathmini ya utendaji, huku mashirika sita yakisimamishwa baada ya kubainika kufanya ukiukaji wa kanuni unaohitaji hatua rasmi za marekebisho.

Wizara imeeleza kuwa mfumo wake wa tathmini unategemea viashiria vya uendeshaji na usimamizi vinavyopima ubora wa huduma pamoja na kiwango cha kuzingatia kanuni. Lengo ni kuimarisha ushindani miongoni mwa watoa huduma na kuinua viwango vya utendaji, ili kuhakikisha mahujaji wa Umrah na wageni wa Msikiti wa Mtume (S.A.W.) wanapata huduma salama na zenye ubora wa juu.

Aidha, wizara imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia kwa ukali utekelezaji wa kanuni, ikibainisha kuwa haitavumilia uzembe au mapungufu yoyote yanayoathiri ubora wa huduma au haki za wanaotekeleza ibada ya Umrah.

Imeongeza kuwa tathmini endelevu ya mashirika ya Umrah ni nyenzo muhimu katika kuendeleza sekta hii na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wageni wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu.

3497830

Kishikizo: umrah saudi arabia
captcha