
Katibu na Msimamizi Mkuu wa Idara ya Awqaf Punjab, Dkt. Ehsan Bhutta, alisema Jumatano kuwa rasilimali zote zilizopo zitatumika kuhakikisha yanaondolewa aina yoyote ya upotoshaji wa maandishi au wa kimaana pamoja na makosa ya uchapishaji katika Qur’ani Tukufu.
Akizungumza katika mkutano wa 59 wa ngazi ya juu wa Bodi ya Qur’ani ya Punjab, Bhutta alitangaza kuanza mara moja kwa kozi maalumu za mafunzo zitakazolenga kuboresha uwezo wa kitaaluma wa wakaguzi wa matini (proofreaders), sambamba na kuandaliwa kwa seti pana ya kanuni elekezi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Qur’ani ya Punjab, Hafiz Zubair Hassan, pamoja na wajumbe mashuhuri wa bodi hiyo.
Katika hotuba yake, Bhutta alitoa maagizo madhubuti ya kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji katika jimbo lote ili kuzuia aina yoyote ya kukashifiwa au kudhalilishwa kwa Qur’ani Tukufu na kuhakikisha hifadhi salama ya nakala zake. Alieleza kuwa hatua hiyo itatekelezwa kupitia ushirikiano wa karibu kati ya utawala wa wilaya na maafisa wa Awqaf.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kufuatilia kwa karibu majukwaa ya mitandao ya kijamii ili kuzuia vitendo vyovyote vyenye nia mbaya vinavyoweza kudhoofisha maelewano ya kidini na ya kijamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Qur’ani ya Punjab, Hafiz Zubair Hassan, alisisitiza kuwa kulinda matini ya Qur’ani Tukufu na kuhakikisha inachapishwa bila dosari kwa kuzingatia roho na uhalisia wake ni jukumu lao kuu la kidini na kisheria. Aliongeza kuwa wajumbe wote wa bodi hiyo wanatekeleza majukumu yao kwa bidii, kujitolea na uaminifu mkubwa.
Ili kuboresha zaidi utendaji wa bodi hiyo, Katibu wa Awqaf alielekeza kuundwa kwa kamati maalumu zitakazojumuisha wajumbe wa bodi ili kusimamia masuala mbalimbali yanayohusiana na Qur’ani. Pia aliamuru kuwasilishwa kwa ripoti ya maandishi kuhusu maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa katika mkutano ujao.
3497798