IQNA

Haramu za Karbala zapambwa kwa bendera nyeusi kuelekea Muharram

17:54 - June 13, 2026
Habari ID: 3482356
IQNA – Kuta na viwanja vya makaburi au haram tukufu za Imam Hussein (AS) na Hadhrat Abbas (AS) katika mji wa Karbala, Iraq, vimepambwa kwa bendera nyeusi na alama za maombolezo huku mwezi wa Muharram wa kalenda ya Hijria ukikaribia.

Utekelezaji wa mpango wa kusimamisha bendera nyeusi na alama za huzuni katika viwanja vya haramu hizo mbili ulianza siku chache zilizopita.

Kwa mujibu wa Abdul Hussein Muhammad, mkuu wa Idara ya Matengenezo ya Haram Takatifu ya Imam Hussein (AS), hatua hizi zinachukuliwa kama maandalizi ya kuukaribisha mwezi wa Muharram na kuandaa majlisi na hafla kubwa za maombolezo kwa kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein (AS), familia yake na masahaba wake waaminifu.

Aliongeza kuwa mpango huo unatekelezwa kwa amri ya moja kwa moja ya mwakilishi wa Marja’iyya ya juu ya kidini, kama ilivyoripotiwa na Al‑Kafeel.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa haramu tukufu inakuwa katika hali bora kabisa, tayari kuwapokea mamilioni ya mazuwaru na waombolezaji watakaokuja Karbala kuadhimisha kumbukumbu ya (shahada ya Imam Hussein (AS)),” alisema.

Kila mwaka inapokaribia mwezi mtukufu wa Muharram, haramu hizi mbili huandaliwa ili kuwapokea wapenzi wa Imam Hussein (AS) kupitia mipango maalumu ya huduma kwa mazuwaru.

Muharram ni mwezi wa kwanza katika kalenda ya Hijria ya Kiislamu.

Waislamu wa madhehebu ya Shia, pamoja na wengine katika sehemu mbalimbali za dunia ya Kiislamu, huandaa kila mwaka majlisi na ibada za maombolezo katika mwezi wa Muharram kwa kukumbuka kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein (AS) na wenzake.

Imam wa tatu wa Shia (AS), pamoja na kundi dogo la wafuasi wake na watu wa familia yake, waliuawa kishahidi na mtawala dhalimu wa zama zake, Yazid bin Muawiya, katika vita vya Karbala mnamo tarehe 10 Muharram , siku inayojulikana kama Ashura , mwaka 61 Hijria sawa  na 680 Miladia.

Mwaka huu, mwezi wa Muharram unatarajiwa kuanza Jumanne, tarehe 16 Juni, huku siku ya Ashura ikiangukia tarehe 25 Juni.

3497813

captcha