IQNA

Wizara ya Wakfu ya Misri yamuenzi Qari marhum Shekh Hilal

16:03 - May 30, 2026
Habari ID: 3482304
IQNA – Wizara ya Awqaf (Wakfu) ya Misri imeuhuisha na kuuenzi ukumbusho wa qari marehemu wa Qur’ani Tukufu, Sheikh Sayyid Abdul Shafi Hilal, katika maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa.

Akitambuliwa kwa lakabu ya “Balozi wa Dola ya Qira’ah”, Sheikh Hilal alikuwa miongoni mwa nguzo kuu katika fani ya usomaji wa Qur’ani Tukufu nchini Misri na katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Al‑Shorouk.

Sheikh Hilal alizaliwa tarehe 29 Mei 1945 katika eneo la Damanhur Shubra Al‑Khaimah, mkoani Qalyubia, Misri, na aliacha nyuma maisha yenye baraka ya khidma katika kulitumikia Neno la Wahyi.

Alikulia katika familia yenye hamasa ya elimu na Qur’ani Tukufu, na aliihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu akiwa bado mdogo.

Alihitimisha hifdhi ya Qur’ani yote akiwa na umri wa miaka 12. Baada ya hapo, alisoma elimu za tajwīd na qirā’āt kwa wanazuoni kadhaa wa Qur’ani; miongoni mwa walimu wake mashuhuri alikuwa Sheikh Muhammad Abdel Ghani, aliyemuelekeza kujiunga na Taasisi ya Qira’ah ya Al‑Azhar ili akamilishe malezi yake ya dini na elimu ya Qur’ani.

Kipaji chake cha qira’ah kilionekana tangu utotoni; na kabla ya kufikisha umri wa miaka 17 alikuwa tayari hushiriki kwenye hafla za maulidi na munasaba za dini, pamoja na “nyusiku za Qur’ani” (layālī al‑Qur’ān), hadi sifa yake ikasikika kote nchini.

Alijulikana kwa sauti yenye nguvu na athari, iliyomweka miongoni mwa ma‑qurra wa kizazi bora cha Misri. Pia alipata cheo cha “Balozi wa Dola ya Qira’ah” kutokana na juhudi zake pana za kueneza Qur’ani Tukufu ndani na nje ya Misri.

Sheikh Hilal alifaulu mitihani ya kujiunga na Redio ya Misri mwaka 1976, baada ya kuwa amejenga utambulisho wake binafsi katika utendaji na usomaji.

Alisisitiza kuwa na mtindo wake mahsusi bila kuiga wengine, hivyo akaacha alama ya pekee kwa hadhira na wapenzi wa Qur’ani.

Sheikh Hilal alikuwa mwakilishi wa Misri katika nchi nyingi duniani; alisafiri zaidi ya nchi 20 za Kiarabu, Ulaya, Afrika na Amerika, na alisoma Qur’ani katika mikusanyiko mikubwa ya Kiislamu. Vilevile, alirekodi Qur’ani Tukufu yote mara mbili nchini Marekani na Uswisi. Inaripotiwa pia kuwa baadhi ya wanaume na wanawake waliingia Uislamu baada ya kuguswa na kusikiliza tilāwa yake ya Qur’ani Tukufu.

Kwa miaka mingi, Sheikh Hilal alishika nafasi ya kiongozi wa ma‑qurra wa mkoa wa Qalyubia, na alitambulika kwa juhudi zake za kuwalea na kuwaongoza wasomaji, akisisitiza uthabiti na ukamilifu wa kanuni za tajwīd. Aliendeleza khidma hii ya kulitumikia Neno la Wahyi hadi alipofariki dunia tarehe 18 Julai 2013, akiacha nyuma urithi wa Qur’ani usiofutika.

4354929

Habari zinazohusiana
captcha