IQNA

Idhaa ya Qur’ani ya Misri Yaaanza Kurusha Tarteel ya Sheikh Minshawi

17:36 - June 03, 2026
Habari ID: 3482318
IQNA – Idhaa ya Qur’ani Tukufu ya Misri, yenye makao yake Cairo, imeanza kurusha hewani usomaji wa Qur’ani kwa mtindo wa tarteel wa miaka ya 1960 wa qari mashuhuri Sheikh Mohamed Siddiq El‑Minshawi.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha maudhui ya Qur’ani na kufufua hazina adimu za redio zinazohifadhiwa katika Idhaa ya Qur’ani.

Katika muktadha huo, Ahmed Al‑Musalmani, Mkuu wa Shirika la Taifa la Habari la Misri, amepongeza juhudi za Idhaa ya Qur’ani Tukufu katika kuhifadhi turathi za Qur’ani za taifa hilo, na akaishukuru familia ya Sheikh Minshawi kwa kuendelea kuunga mkono redio hiyo na kuwezesha usambazaji wa kisomo adimu cha marehemu qari huyo kwa umma.

Ismail Douidar, Mkuu wa Idhaa ya Qur’ani Tukufu, amesema kuwa kurushwa kwa kisomo hicho ni sehemu ya mkakati wa chombo hicho cha habari wa kuimarisha vipindi vyake kwa “lulu za milele” na kufafanua vipengele vya kipekee vya kitaaluma na kibinadamu katika maisha ya wasomaji maarufu wa Qur’ani.

Ameeleza kuwa baada ya kupata idhini ya kamati maalumu iliyojumuisha wanazuoni mashuhuri wa qira’aat na tajwid, Ustaadh Minshawi, kwa kushirikiana na Mhandisi Farouk Amer, alirekodi Qur’ani Tukufu yote kwa mtindo wa tarteel kwa riwaya ya Hafs ‘an ‘Asim mwaka 1965.

Mkuu huyo wa Idhaa ya Qur’ani amesisitiza kuwa rekodi hizo hazikuwa zimewahi kurushwa hewani kwa miongo kadhaa, hadi uongozi wa sasa ulipoamua kuzitangaza, ili kuwapa wasikilizaji tajriba ya kiroho iliyo ya kipekee na kuonyesha ikhlasi na juhudi za Sheikh Minshawi katika kukamilisha usomaji wa Qur’ani Tukufu kwa ukamilifu wake.

Sheikh Mohamed Siddiq El‑Minshawi anahesabiwa miongoni mwa maqari wa zama za dhahabu za usomaji wa Qur’ani nchini Misri.

Alizaliwa tarehe 20 Januari 1920 katika mji wa Minshat, mkoa wa Sohag, Misri, na alikulia katika familia yenye uchamungu na elimu ya dini. Akiwa na umri wa miaka minane tu, alikuwa tayari ameihifadhi Qur’ani Tukufu yote.

Katika kipindi cha huduma yake, alisoma Qur’ani mara nyingi ndani na nje ya Misri, ikiwemo katika maeneo matakatifu kama Al‑Masjid Al‑Haram, Al‑Masjid An‑Nabawi, na Msikiti wa Al‑Aqsa kabla haujakaliwa kwa mabavu.

Sheikh Minshawi pia alisafiri katika nchi mbalimbali kama Kuwait, Syria, Libya na Indonesia, ambako alipokea heshima na tuzo nyingi kwa mchango wake katika huduma ya Qur’ani Tukufu.

Qari huyu wa Misri alifariki dunia tarehe 20 Juni 1969 akiwa na umri wa miaka 49.

3497699

captcha