IQNA

Misikiti 15 yafungwa Arunachal Pradesh, India na kuzua malalamiko ya Waislamu

17:44 - June 13, 2026
Habari ID: 3482355
IQNA – Mamlaka katika mji mkuu wa jimbo la Arunachal Pradesh nchini India zimezifunga misikiti yote 15 iliyoko katika mji huo mkuu, hatua iliyozua ukosoaji na malalamiko kutoka kwa makundi ya Kiislamu.

Viongozi wa jamii ya Waislamu wamesema hatua hiyo ni ya kibaguzi na kudai kuwa inaashiria kuongezeka kwa shinikizo dhidi ya taasisi za Kiislamu katika eneo hilo.

Hatua ya serikali ya jimbo inayoongozwa na chama cha BJP imekuja baada ya kuitishwa kwa mgomo wa jumla (bandh) na shirika la Arunachal Pradesh Indigenous Youth Organization (APIYO), kundi la vijana wenye msimamo wa utaifa wa kikabila, ambalo lilitaka mamlaka zichukue hatua dhidi ya kile walichokiita misikiti “isiyo halali” katika mji huo.

Baada ya kufungwa kwa misikiti hiyo, utawala wa wilaya ulitoa taarifa ukisema kuwa Naibu Kamishna pamoja na Hakimu Mtendaji (Assistant Commissioner‑cum‑Executive Magistrate) wameamuru kufungwa kwa misikiti yote katika eneo la Itanagar Capital Region, ikiwemo Msikiti wa Jama Masjid. Inaripotiwa kuwa mamlaka zimedai majengo hayo ya ibada yalikuwa yakifanya kazi bila vibali vya kisheria vinavyotakiwa.

Kamati ya Ustawi wa Misikiti ya Arunachal Pradesh (All Arunachal Pradesh Masjid Welfare Committee – AAPMWC) imetoa wito kwa mamlaka kufungua tena misikiti hiyo, huku ikihoji kile ilichokitaja kuwa ni utekelezaji wa sheria kwa namna ya kuchagua upande mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari, mwanachama wa AAPMWC, Giah Limpeh Sultan, alisema kuwa ikiwa mamlaka zinachunguza uhalali na nyaraka za misikiti, basi viwango hivyo hivyo vinapaswa kutumika pia kwa taasisi za kidini za jamii zote.

“Mamlaka zinachunguza uhalali na nyaraka za misikiti katika eneo la mji mkuu. Uchunguzi huo huo unapaswa pia kufanywa kwa makanisa, gurudwara, namghar, mahekalu na majengo mengine ya ibada ambayo huenda yanafanya kazi bila vibali kamili vya kisheria au nyaraka zinazohitajika,” alisema Sultan.

Kamati hiyo ilifafanua kuwa haipingi ufuataji wa sheria, lakini inapinga kile inachokiona kama kutokuwepo kwa usawa katika utekelezaji wake. Kwa mujibu wa Sultan, taarifa zilizopatikana kupitia Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa (Right to Information – RTI) zinadaiwa kuonyesha kuwa baadhi ya majengo ya ibada ya jamii nyingine pia yanafanya kazi bila vibali kamili.

Baadhi ya wanajamii wa Kiislamu wanasema kufungwa kwa misikiti hiyo ni sehemu ya mwenendo mpana wa shinikizo linaloongezeka dhidi ya taasisi za Kiislamu katika mji wa Itanagar.

Mkazi mmoja wa eneo hilo anayehusishwa na shughuli za msikiti, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alidai kuwa wanachama wa APIYO hapo awali walikuwa wamepinga kuwepo kwa maktab, vituo vidogo vya kujifunzia dini ya Kiislamu ambako watoto hupata mafundisho ya dini.

“Walituuliza kwa nini tunaendesha madrasa hapa. Tukawaeleza kuwa hizi si madrasa bali ni maktab,” alisema mkazi huyo.

Kwa mujibu wake, maktab 11 kati ya 14 zilizokuwa katika eneo hilo hatimaye zilifungwa baada ya wamiliki wa majengo kudaiwa kuwekwa chini ya shinikizo ili wasiruhusu tena shughuli hizo kufanyika.

Wanajamii pia wamepinga madai kuwa misikiti hiyo ni haramu. Wamesema majengo mengi yalijengwa kwa miaka kadhaa kupitia michango ya waumini, na katika baadhi ya matukio kwa idhini ya wamiliki wa ardhi wa eneo hilo.

Baadhi ya kamati za misikiti zimesema kuwa tayari ziliwasilisha maombi ya kupangiwa ardhi rasmi, huku nyingine zikidai kuwa zimekuwa zikiwasilisha mara kwa mara nyaraka kwa mamlaka husika ili kupata vibali vya kisheria.

Afisa mwingine wa msikiti alisema kuwa Waislamu wengi katika jimbo hilo husita kupinga hadharani kufungwa kwa misikiti hiyo kwa hofu ya kuitwa “wageni” au “watu wa nje” na kisha kukabiliwa na shinikizo la kijamii au kisiasa.

Katika jimbo la Arunachal Pradesh, mijadala kuhusu utambulisho wa asili ya wenyeji, uhamiaji na haki za ardhi imekuwa suala nyeti kisiasa kwa miaka mingi, mara nyingi ikiathiri mvutano wa kijamii na maamuzi ya sera za eneo hilo.

Ingawa mamlaka zimesisitiza kuwa misikiti hiyo imefungwa kutokana na kukosa vibali vya kisheria, hadi sasa hakujatolewa majibu ya kina hadharani kuhusu madai ya kuchagua upande mmoja yaliyotolewa na mashirika ya Kiislamu.

3497817

Kishikizo: india waislamu bjp
captcha