IQNA

Siri ya kudumu kwa Sauti ya Qari mashuhuri wa Misri, Sheikh Mohamed Siddiq Al‑Minshawi

15:45 - June 14, 2026
Habari ID: 3482359
Siri ya kudumu kwa Sauti ya Qari mashuhuri wa Misri, Sheikh Mohamed Siddiq Al‑Minshawi
IQNA – Kisa hiki kinaanza katika miaka ya 1960, pale Sheikh Mohamed Siddiq Al‑Minshawi aliporekodi usomaji wa Qur’ani Tukufu yote kwa ajili ya Redio au Idhaa ya Qur’ani ya Misri.

Kilichotangazwa hivi karibuni na Idhaa ya Qur’ani ya Misri si tu rekodi za zamani zilizotolewa kutoka katika maktaba ya kumbukumbu, bali ni ugunduzi mpya wa sauti ambayo, licha ya mwenye nayo kufariki dunia miongo kadhaa iliyopita, imeendelea kubaki hai katika nyoyo za mamilioni ya watu, kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera.

Tangu usomaji huo adimu wa Qur’ani wa qari huyo marehemu wa Misri uanze kurushwa hewani, rekodi hizo mpya zimekuwa zikiongoza mijadala kwenye mitandao ya kijamii nchini humo. Jina la Minshawi limeendelea kuwa miongoni mwa mada zinazozungumzwa kwa siku kadhaa mfululizo, hata kuzidi matukio makubwa ya michezo na habari. Hali hii imefufua swali la zamani: ni ipi siri inayofanya sauti hii iendelee kuishi zaidi ya nusu karne baadaye?

Kisa chenyewe kilianza katika miaka ya 1960, wakati Minshawi aliporekodi Qur’ani yote kwa ajili ya Idhaa ya Qur’ani. Ingawa kamati ya tathmini iliidhinisha na kuisifu rekodi hiyo, qari huyo mashuhuri hakuridhika. Baada ya kusikiliza rekodi hizo, alihisi baadhi ya kanda hazikufikia kiwango alichokitaka, hivyo akawasilisha ombi rasmi la kurekodi upya baadhi ya sehemu.

Katika hatua nadra iliyoonesha umakini wake mkubwa na kujitolea kwake kwa ukamilifu wa kisanaa katika usomaji wa Qur’ani, Minshawi aligharamia binafsi kurekodi upya kanda 32 kati ya kanda 82 zilizounda usomaji kamili wa Qur’ani. Baada ya kukamilika, kamati iliidhinisha rasmi toleo hilo jipya mwaka 1967.

Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kwamba toleo hili halikuwahi kufikishwa kwa umma; badala yake, lilibaki limehifadhiwa katika kumbukumbu za redio kwa miongo kadhaa.

Maswali Yasiyoweza Kupuuziwa

Sheikh Ahmed Issa Al‑Masrawi, aliyewahi kuwa mkuu wa Mamlaka ya Usomaji wa Qur’ani nchini Misri, anaamini suala hili linaibua maswali muhimu yasiyoweza kupuuzwa. Alisisitiza kuwa Minshawi hakuomba kurekodi upya bila sababu, bali alifanya hivyo kwa sababu alitaka kufikia kiwango cha juu zaidi cha utendaji katika qiraa.

Al‑Masrawi alisema kuwa sheikh huyo “alifanikiwa kufikia lengo hilo katika kanda alizorekodi upya.” Aliongeza kuwa aliposikiliza toleo jipya, aligundua “upole na hali ya kiroho katika sauti yake ambavyo havikuonekana katika rekodi zilizokuwa zikirusha kwa miongo kadhaa.”

Alisisitiza kuwa tofauti kati ya matoleo hayo mawili ni wazi kabisa, akieleza kwamba rekodi mpya zinatambulika kwa “sauti yenye mwangaza, utendaji wenye nguvu, na kiwango cha juu sana cha uzuri pamoja na hali ya kiroho.”

Kwa mujibu wa Al‑Masrawi, sifa hizi zinaonekana wazi kwa yeyote anayelinganisha na rekodi zilizotangazwa hapo awali.

Hata hivyo, jambo lililomshangaza zaidi ni kwa nini kanda hizi zilifichwa kwa muda mrefu kiasi hicho. Ikiwa Minshawi mwenyewe aliomba kurekodi upya, redio ilikubali, na kamati ikaidhinisha rasmi toleo jipya, kwa nini rekodi hizi zilibaki kwenye kumbukumbu kwa karibu miaka sitini?

Alisema swali hili limekuwa likimsumbua tangu aliposikiliza rekodi hizo mpya, akibainisha kuwa kuchelewa kwa kutolewa kwake kunazua maswali mengi kuhusu hatima ya rekodi nyingine ambazo huenda bado zimo katika maktaba za kumbukumbu.

Al‑Masrawi pia hakuweza kuficha mshangao wake kuhusu tetesi zinazosambaa kuhusu uwepo wa qiraa nyingine adimu za Minshawi zenye riwaya tofauti. Alithibitisha kuwa hapo awali aliwahi kusikia baadhi ya rekodi ambazo hazijawahi kutolewa, na hata alipokea kanda za moja ya qiraa zilizotangazwa hivi karibuni miaka kadhaa iliyopita, jambo linaloashiria kuwa sehemu yake ilikuwa tayari inasambaa katika mzunguko mdogo.

Hakutilia shaka tu sababu za kuchelewa kwa matangazo ya qiraa hiyo mpya, bali pia alihusisha jambo hilo na matukio mengine yaliyotokea katika kumbukumbu za Redio ya Misri, akisema kuwa kilichotokea kinaonekana kana kwamba kilifanywa kwa makusudi.

Alitoa mfano wa tajriba ya qari marehemu Mahmoud Khalil Al‑Husari, ambaye alirekodi qiraa kwa riwaya ya Al‑Duri kutoka kwa Abu Amr, pamoja na Warsh na Qalun, katika miaka ya 1963 na 1964, lakini rekodi hizo hazikutolewa hadharani hadi mwaka 2001.

Aliongeza: “Hivi karibuni nilivutiwa na machapisho kwenye mitandao ya kijamii ya Fadia, binti wa Sheikh Minshawi, ambaye alizungumzia kutolewa hivi karibuni kwa qiraa nyingine adimu za baba yake kwa riwaya ya Shu’bah kutoka kwa Asim, Warsh kutoka kwa Nafi, na Al‑Duri kutoka kwa Abu Amr — rekodi ambazo hata yeye hakujua uwepo wake kwa miaka mingi.”

Kwa mujibu wa Al‑Masrawi, kufichuliwa kwa taarifa hizi sasa kunazua maswali zaidi kuhusu rekodi zipi nyingine bado zimehifadhiwa katika maktaba ambazo hazijawahi kufichuliwa. “Hili ni jambo la kitendawili, na sielewi kwa nini linatokea sasa,” alisema.

Hata hivyo, maneno ya Al‑Masrawi hayakuhusu tu rekodi zilizofichwa au zilizosahaulika; pia yaligusa siri ya nafasi ya kipekee ya Minshawi katika nyoyo za wasikilizaji.

Kwa mujibu wake, Minshawi hakuwa tu msomaji hodari wa Qur’ani au mwenye sauti nzuri, bali aliunganisha kwa pamoja ubora wa utendaji, umakini mkubwa, ustadi, uzuri wa sauti, na kina cha hali ya kiroho.

Alisema kuna “roho ya Qur’ani” ya kipekee katika qiraa ya Minshawi ambayo haioni kwa msomaji mwingine yeyote, hata miongoni mwa majina makubwa ya shule ya wasomaji wa Qur’ani ya Misri.

Akibainisha kuwa miaka ya hivi karibuni imethibitisha kuwa umaarufu huu wa kipekee haujapungua, Al‑Masrawi alisema, “Ni vigumu kuingia mahali na usisikie sauti ya Sheikh Minshawi,” kwa sababu Mwenyezi Mungu alimjaalia msomaji huyu kukubalika kwa namna ya pekee isiyolinganishwa na qari mwingine yeyote.

Alipoulizwa ni sauti ipi kati ya wasomaji wakubwa wa Qur’ani wa Misri iliyo karibu zaidi na moyo wake, alijibu bila kusita: “Sheikh Minshawi,” akieleza kuwa sauti yake inaunganisha sifa ambazo ni nadra kupatikana kwa wengine: ustadi, uwasilishaji wenye uzuri, na hali ya kiroho inayogusa moyo kabla hata ya masikio.

Huenda kwa sababu hiyo, kutolewa upya kwa rekodi hii adimu kumekuwa tukio la kipekee nchini Misri na ulimwengu wa Kiarabu. Haikuwa tu kuachiliwa kwa rekodi za zamani, bali ni kufufuliwa kwa sauti ambayo wengi bado wanaiona kuwa miongoni mwa kilele cha sanaa ya qiraa katika zama za kisasa — na kwamba kanda hizi mpya zilizotolewa ni mwangwi wa kuchelewa wa mtu aliyekuwa akitafuta ukamilifu katika usomaji wa Qur’ani, huku athari yake ikiendelea kusikika masikioni mwa wasikilizaji hata miaka sitini baada ya kifo chake.

3497822

Habari zinazohusiana
Kishikizo: Minshawi misri qari
captcha