
Maukibu ni vituo vya huduma za kujitolea vinavyotoa chakula, malazi, na misaada ya kitabibu bila malipo kwa wafanyaziara na waombolezaji.
Idara ya Husseini na Misafara ya Maombolezo, iliyo chini ya Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS), imetangaza kutolewa kwa vibali 746 kwa ajili ya kuanzisha maukibu zitakazohudumu katika hafla za maombolezo ya Ashura.
Idara hiyo pia ilisema kuwa maukibu 14,000 zitawahudumia mazuwaru katika msafara wa Arabaeen wa mwaka huu.
Mkuu wa idara hiyo, Mohammad Karim Aziz, amesema katika mahojiano na Shirika la Habari la Noon kwamba idara yake imekamilisha maandalizi ya awali kwa ajili ya kuhuisha siku kumi za mwanzo za Muharram na ibada za maombolezo ya Ashura.
Alibainisha kuwa kamati maalumu imeundwa kwa ajili ya kuratibu utoaji wa vibali rasmi.
Aziz alisema kuwa hatua hiyo ilifuata kikao kilichofanyika kwa ushiriki wa Sheikh Abdul Mahdi Al-Karbalai, Hassan Rashid Al-Abaji, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi, pamoja na wakuu wa idara mbalimbali.
Kwa mujibu wake, katika kikao hicho walikubaliana juu ya maandalizi ya siku kumi za mwanzo za Muharram.
Aliongeza kuwa programu hizo zitaanza katika usiku wa kuandama mwezi wa Muharram kwa hafla ya kubadilisha bendera ya maombolezo, na zitaendelea hadi siku ya kumi kwa shughuli za Tuwairij.
Siku ya Ashura ni siku ya kumi ya mwezi wa Kiislamu wa Muharram, na ni siku ya maombolezo kwa kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS) na masahaba zake katika Vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.
Mwaka huu, Ashura itaangukia siku ya Alhamisi, 15 Juni.
3497787