IQNA

Waislamu wa China

Msikiti Mkuu wa Taipei wahifadahi utambulisho wa Kiislamu eneo la China la Taiwan

15:48 - June 07, 2026
Habari ID: 3482333
IQNA – Kwa kutegemea mradi wa kielimu ulioendelea kwa zaidi ya miaka ishirini, Msikiti Mkuu au Msikiti wa Jamia wa Taipei katika eneo la China la Taiwan umejidhihirisha kama mfano wenye mafanikio katika kulea na kuelimisha vizazi vijavyo vya Waislamu.

Katika msikiti huu, wanafunzi wa jana, leo wamekuwa walimu na wahudumu wa kujitolea, wakichukua jukumu la kuendeleza elimu ya dini kwa kizazi kipya ili mnyororo wa kurithishana utambulisho wa Kiislamu usikatike kamwe.

Ndani ya jamii ndogo ya Kiislamu inayokua polepole katika mazingira ya uhuru wa dini, uwazi wa kijamii na mshikamano katika Asia ya Mashariki, kuna swali muhimu linalozidi mipaka ya elimu ya kawaida: Je, utambulisho wa Kiislamu unaweza kuhifadhiwaje na kurithishwa bila kukatika kutoka kizazi kimoja hadi kingine?

Jibu la swali hili linaonekana wazi katika tajriba ya Msikiti Mkuu wa Taipei. Huu ni mradi wa kielimu uliodumu kwa zaidi ya miongo miwili, ambapo watoto waliowahi kujifunza Qur’ani Tukufu na misingi ya Uislamu katika msikiti huo sasa wamekuwa walimu na wahudumu wanaorudi kuwafundisha watoto wa kizazi kipya.

Hafla ya kufunga mwaka wa masomo wa 2025–2026 wa madrasa ya kila wiki ya msikiti huo imeonesha kuwa mafanikio ya kweli hayapimwi kwa idadi ya wanafunzi au vyeti vinavyotolewa, bali kwa uwezo wa kuunda mzunguko endelevu wa elimu. Baadhi ya walimu wa leo wanahudumu katika nafasi zilezile walizokuwa wakikaa miaka iliyopita kama wanafunzi wadogo waliokuwa wakipokea elimu na malezi.

Mfumo huu wa elimu unawakilisha jaribio muhimu la kuhifadhi elimu ya Kiislamu ndani ya jamii ya Waislamu wa eneo la Taiwan nchini China. Shule hii inaunganisha mafundisho ya Qur’ani Tukufu, lugha ya Kiarabu na masomo ya Kiislamu pamoja na kuwalea watu wenye uwezo wa kubeba na kueneza ujumbe wa Uislamu kwa vizazi vijavyo, hivyo kudumisha utambulisho wa Kiislamu na kuimarisha uwepo wake kizazi baada ya kizazi.

Msikiti Mkuu wa Taipei uliandaa hafla ya kufunga madrasa ya kila wiki kwa watoto na vijana, ambapo wanafunzi walitunukiwa vyeti na zawadi mbalimbali. Hata hivyo, jambo lililovutia zaidi lilikuwa uwepo wa walimu na wahudumu kadhaa waliowahi kusoma katika madarasa hayo hayo miaka iliyopita.

Hali hii inaonesha mafanikio ya shule hiyo katika kufikia lengo linalozidi mipaka ya elimu ya kawaida: kuwalea wanajamii wa Kiislamu ili baadaye wawe sehemu ya mchakato wa elimu wenyewe, na hivyo kuhakikisha uendelevu wa kurithishana maarifa, maadili na tajriba kati ya vizazi.

Kwa zaidi ya miaka ishirini, madrasa hii ya kila wiki imekuwa ikitekeleza jukumu lake kwa kutoa programu za elimu kwa watoto na vijana katika nyanja za Qur’ani Tukufu, lugha ya Kiarabu, utamaduni wa Kiislamu na malezi ya maadili.

Kwa muda wa miaka hiyo, athari za programu hii hazijaishia tu katika kuhitimisha makundi mapya ya wanafunzi, bali pia imezalisha kizazi cha vijana kutoka ndani ya msikiti wenyewe, ambao baadhi yao wamekuwa wakirudi baada ya miaka kadhaa kushiriki katika ufundishaji, usimamizi na kazi za kujitolea. Hali hii inaipa mradi huu mwelekeo wa kimkakati unaovuka mipaka ya elimu ya moja kwa moja.

Programu hii imejengwa juu ya falsafa ya kielimu inayotanguliza malezi ya Kiislamu, adabu na tabia njema, kwa kuamini kwamba kujenga haiba ya Mwislamu kunatangulia kupata maarifa na ujuzi.

Kwa hiyo walimu hujitahidi kuwafundisha watoto heshima kwa msikiti na Qur’ani Tukufu, nidhamu, ushirikiano na uwajibikaji sambamba na mafundisho ya elimu za Kiislamu. Hili huwasaidia watoto kukuza utambulisho wa Kiislamu ulio thabiti na wenye uwiano, unaoweza kuishi kwa maelewano na jamii inayowazunguka.

Nafasi ya Wahudumu wa Kujitolea katika Kudumisha Elimu ya Kiislamu

Shule hii pia inanufaika na ushiriki wa walimu na wahudumu wa kujitolea kutoka asili mbalimbali za kitamaduni, wakiwemo wazungumzaji wa Kichina, Waislamu wapya na wanachama wa jamii ya Kiislamu wanaoishi Taiwan.

Eneo hilo la kitamaduni huimarisha na kupanua mchakato wa elimu, na huwapa watoto fursa ya kujifunza utofauti wa ulimwengu wa Kiislamu ndani ya mazingira moja ya kielimu yanayochanganya uhifadhi wa utambulisho na uwazi kwa jamii.

Jamii ndogo za Kiislamu mara nyingi hukabiliwa na changamoto ya kuhakikisha kuwa elimu ya dini na maadili ya Kiislamu yanarithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Hata hivyo, tajriba ya Msikiti Mkuu wa Taipei inatoa mfano halisi wa jinsi changamoto hii inaweza kushughulikiwa kupitia uwekezaji wa muda mrefu katika watoto na vijana.

Watoto wanaoelimishwa leo wanaweza kuwa walimu wa kesho, na wahudumu wa kujitolea wanaohudumu leo mara nyingi ni wahitimu wa programu hiyo hiyo. Hali hii huunda mzunguko endelevu wa kujifunza na kutoa huduma, unaosaidia kuhifadhi utambulisho wa Kiislamu na kuziwezesha jamii za Kiislamu kukua na kustawi.

Taiwan ni kisiwa cha China kilichoko Asia ya Mashariki chenye idadi ya watu takriban milioni 23. Inakadiriwa kuwa Waislamu nchini humo ni karibu laki tatu. Msikiti Mkuu wa Taipei ni miongoni mwa taasisi muhimu zaidi za Kiislamu nchini humo na kituo kikuu kinachotoa huduma za kidini, kielimu na kitamaduni kwa jamii ya Kiislamu.

Tajriba hii inaonesha kuwa mafanikio ya taasisi za Kiislamu hayapimwi kwa idadi ya shughuli au sherehe wanazoandaa, bali kwa uwezo wao wa kuandaa vizazi vipya vitakavyoendeleza kujenga na kuhifadhi urithi na utambulisho wa Kiislamu katika siku zijazo.

3497737

captcha