IQNA

Tani 235 za Maji ya Zamzam husambazwa kila siku katika Al Masjid An Nabawi

18:04 - June 12, 2026
Habari ID: 3482353
IQNA – Kila siku, tani 235 za maji ya Zamzam husambazwa katika Al Masjid An Nabawi (Msikiti wa Mtume (SAW)) mjini Madina.

Kwa mujibu wa Urais Mkuu wa Masuala ya Masjid Al Haram mjini Makka na Al Masjid An Nabawi mjini Madina, huduma za usambazaji wa maji kwa mahujaji na wageni hutolewa kupitia mfumo wa uendeshaji unaofanya kazi saa 24.

Taasisi hiyo imeweka upatikanaji wa maji ya Zamzam katika maeneo mbalimbali ndani ya msikiti na katika viwanja vyake vya nje.

Urais huo umeongeza kuwa mfumo huo hutumia takribani vikombe vya plastiki 796,000 kila siku, huku kiasi cha maji ya Zamzam kinachosambazwa na kutumiwa katika Msikiti wa Mtume kikifikia takribani tani 235 kwa siku ili kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya waumini na wageni.

Mfumo wa usambazaji wa maji unajumuisha zaidi ya matenki 10,000 yaliyowekwa katika maeneo mbalimbali ya msikiti na viwanja vyake, ambayo hujazwa na kufuatiliwa mara kwa mara. Aidha, vipimo vya mara kwa mara hufanywa kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuhakikisha ubora na usalama wa maji hayo.

Urais huo pia umeweka vituo maalumu vya maji ndani ya Al Masjid An Nabawi, vikiwemo vifaa vya kutoa maji baridi na yasiyo baridi katika baadhi ya milango ya kuingilia na pia juu ya paa la msikiti katika milango ya kutokea namba 25, 29 na 34 kwa maji baridi, na katika lango namba 8 kwa maji yasiyo baridi. Hatua hii inalenga kurahisisha upatikanaji wa maji ya Zamzam kwa waabudu na wageni katika maeneo mbalimbali ya msikiti.

Juhudi hizi zinasemekana kuwa ni sehemu ya mfumo mpana wa huduma unaolenga kukidhi mahitaji ya mahujaji wanaotembelea Al Masjid An Nabawi  na kuwapatia huduma zenye ubora wa hali ya juu zinazoboresha tajriba yao ya kiroho.

 

3497792

Habari zinazohusiana
captcha