Kiongozi Muadhamu aliyasema hayo jana Jumatano alipokutana na Rais Hassan Rouhani na baraza lake la mawaziri kwa mnasaba wa Wiki ya Serikali, ambapo sambamba na kumuenzi Shahid Muhammad Ali Rajai na Muhammad Jawad Bahonar, rais na waziri mkuu wa zamani nchini hapa waliouawa shahidi, amesema kuwa, kuenzi misingi ya Mapinduzi na kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, ni mambo muhimu yaliyokuwa yakipewa umuhimu na mashahidi hao wawili. Ayatullah Khamenei amesifu ripoti ya Rais Rouhani kuhusu utendaji wa serikali yake katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kusema kuwa, ripoti hiyo inatakiwa kuwekwa wazi mbele ya jamii ya Wairan, ili kwamba sanjari na wananchi kuwa na taarifa kamili za mafanikio hayo, waweze pia kujua mipango inayotarajiwa kutekelezwa na serikali hapo baadaye. Kiongozi Muadhamu amelitaja suala la fitina na wafitini kuwa miongoni mwa kadhia inayotakiwa kuzingatiwa na ambayo ni mstari mwekundu na kusema kuwa, wajumbe wa baraza la serikali lazima wafungamane na ahadi zao walizozitoa katika kikao cha kuwapigia kura za kuwa na imani nao bungeni juu ya kujitenga na wafitini. Aidha ameutaja uchapakazi wa serikali ya sasa katika kufuatilia masuala ya kieneo na kimataifa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kuwa ni mzuri na kuitaka serikali kufuatilia kadhia muhimu kama vile ya Palestina, utawala haramu wa Kizayuni, Ghaza, Syria, Iraq, makundi ya kitakfiri na uingiliaji wa Kimarekani katika masuala mbalimbali kwa manufaa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha amesisitiza juu ya utekelezwaji wa siasa za uchumi wa muqawama kwa lengo la kuboresha hali ya ndani na kuzidishwa juhudi za uzalishaji bidhaa za ndani hapa nchini.