IQNA

al Azhar yalaumiwa kwa kukataa kuwapokea wanafunzi Wakristo

10:34 - November 04, 2008
Habari ID: 1704313
Wahadhiri wa Chuo Kukuu cha al Azhar nchini Misri wamepinga hatua ya uongozi wa chuo hicho ya kukataa kuwapokea wanafunzi wa Kikristo na wamewataka viongozi wake kulegeza kamba katika kadhia hiyo.
IQNA imenukuu habari ya kanali ya televisheni ya al Arabiya kwamba Wakili wa Kanisa la Wakristo wa Misri (Coptic Church) Mamduh Nakhla amewasilisha mashtaka dhidi ya Chuo Kikuu cha al Azhar akidai kwamba, chuo hicho kimekiuka katiba ya nchi kwa kufanya ubaguzi kati ya Waislamu na Wakristo.
Katika upande mwingine Mkuu wa Chuo Kikuu cha Darul Ulum cha Cairo amemkosoa Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar kwa hatua hiyo na kusema kuwa, kitendo cha kuwakataa wanafunzi Wakristo kinapingana na uhuru wa fikra unaohubiriwa na dini ya Kiislamu.
Hatua ya Chuo Kikuu cha al Azhar pia imepingwa na mhadhiri wa sheria za Kiislamu katika Chuo Kikuu cha al Zaqaziq Abdulatif A’mir ambaye amesema, sheria za kidini hazikatazi kusajili wanafunzi Wakristo katika vyuo vikuu vya taaluma za Kiislamu na kwamba kitendo hicho kitazidisha taswira mbaya inayoenezwa dhidi ya Uislamu katika miaka ya hivi karibuni.
Hata hivyo Mkuu wa kitengo cha mafunzo ya wafanyakazi wa al Azhar Hussein Auda ametetea hatua hiyo akisema kuwa imechukuliwa kulinda utambulisho wa Kiislamu wa chuo hicho kikongwe zaidi cha taaluma za Kiislamu duniani. Hussein Auda amesema, mada ya 103 ya hati ya mwaka 1961 inayoeleza masharti ya kusajiliwa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha al Azhar inasisitiza kwamba, Waislamu waliohitimu masomo katika sekondari za al Azhar au Waislamu waliohitimu vyuo vikuu ndio wanaoweza kusajiliwa chuoni hapo. 315045
captcha