IQNA

Mlipuko mkubwa watikisa eneo la viwanda la 'Israel' karibu na Al-Quds

15:31 - May 17, 2026
Habari ID: 3482248
IQNA – Mlipuko mkubwa umetokea katika kituo cha viwanda katika eneo la Beit Shemesh karibu na mji mtakatifu wa Al‑Quds (Jerusalem), huku mtikisiko wake ukihisiwa katika maeneo mbalimbali ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la 'Israel'.

Vyombo vya habari vya utawaa wa Israel vilithibitisha kutokea kwa tukio kubwa la kiusalama usiku wa Jumamosi. Hata hivyo, asili halisi ya mlipuko huo bado haijathibitishwa, na mamlaka husika hazijatoa taarifa rasmi kuhusu kilichotokea.

Kampuni ya Tomer ya utawala wa Israel, ambayo ni miongoni mwa taasisi muhimu zinazohusika na maendeleo ya mifumo ya roketi na makombora kwa ajili ya majeshi ya utawala huo, iliharakisha kutoa taarifa ikidai kuwa mlipuko huo haukuwa chochote zaidi ya “jaribio lililopangwa mapema” lililofanyika “kulingana na mpango.”

Taarifa hiyo, iliyonukuliwa na chombo cha habari cha Kan, ilionekana kujaribu kupunguza uzito wa tukio hilo lililotokea katika moja ya maeneo nyeti ya kijeshi ya utawala huo.

Hata hivyo, video nyingi zilizosambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii zinaonyesha taswira tofauti. Picha za video zinaonyesha mlipuko mkubwa uliosababisha wingu kubwa la moshi lililopaa juu angani kama uyoga mkubwa, likionekana kutoka umbali mrefu na kufanana na athari za ajali kubwa katika kituo cha kutengeneza silaha.

Ukubwa wa mlipuko huo umeibua maswali mazito kuhusu hali halisi ndani ya sekta ya kijeshi na viwanda ya Israel, ambayo imekuwa chini ya shinikizo linaloongezeka huku utawala wa Kizayuni ukiendelea na kampeni zake za kijeshi katika maeneo mbalimbali ya kanda.

Vituo vya aina hii, vinavyohusika na utengenezaji wa mifumo ya msukumo kwa makombora na mifumo ya kuyazuia, kwa kawaida hufanya kazi katika mazingira ya usiri mkubwa kutokana na wasiwasi wa mara kwa mara wa usalama pamoja na shinikizo la kudumu kutoka kwa mhimili wa muqawama.

Jeshi na polisi wa utawala wa Israel walikaa kimya kwa muda kabla ya hatimaye kutolewa kwa taarifa iliyopangwa kwa uangalifu kutoka kwa kampuni ya Tomer.

3497485

captcha