IQNA

Ofisi ya Kuhifadhi Qur’ani yafunguliwa rasmi Sinai, Misri

14:03 - May 15, 2026
Habari ID: 3482239
IQNA – Ofisi ya Amal ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu imezinduliwa rasmi katika hafla maalumu iliyoandaliwa katika Mkoa wa Sinai, nchini Misri.

Uzinduzi huo umefanywa na Meja Jenerali Khaled Mujawar, Gavana wa Sinai Kaskazini, katika mji wa Hasna uliopo Sinai ya Kati.

Hatua hii ni sehemu ya jitihada za serikali ya Misri za kuimarisha uelewa wa dini na kukuza maendeleo ya binadamu kupitia malezi bora ya Kiislamu.

Gavana alifuatana na Marzuk Raziq Salem, Mwenyekiti wa Baraza la Jiji la Hasna, Walid Amin Abdel Hamid, Katibu wa Baraza la Jiji, pamoja na kundi la masheikh, viongozi wa koo za Sinai ya Kati na maafisa mbalimbali wa utendaji.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi, Mujawar alikutana na watoto na wanafunzi waliojiandikisha katika kituo hicho na kuwapatia zawadi na vibahasha vya tunzo ili kuwahamasisha zaidi.

Akizungumza katika hotuba yake, Gavana alisisitiza umuhimu wa vituo vya kuhifadhi Qur’ani, akibainisha kuwa kuhifadhi Kitabu Kitukufu ni ngome madhubuti kwa watoto wa Sinai.

“Jambo hili si tu kuwaingiza katika malezi mema na maadili yenye ustahamilivu ya Uislamu, bali pia huchangia pakubwa katika kuunda tabia na mwenendo wao ili waweze kukabiliana na changamoto na kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa lisilo na misimamo mikali.”

Akiendelea, Gavana alimpongeza uongozi wa Kituo cha Amal kwa jitihada zao, na akasisitiza kuwa mkoa utatoa msaada kamili kwa mipango yote inayolenga kueneza elimu sahihi ya dini na utamaduni wa Kiislamu katika miji na vijiji vya Sinai.

Pia alibainisha kuwa wananchi wa Sinai ndio kiini cha maendeleo ya eneo hilo, na akaongeza kuwa ofisi yake iko wazi wakati wote kusikiliza mahitaji na maoni ya watu katika kila sehemu ya mkoa huo.

3497461

captcha