Wanachuo kutoka nchi mbalimbali za dunia wameshiriki katika Duru ya Pili ya Mashindano ya Kimataifa ya Wanachuo wa Kiislamu ya Tehran, mashindano ambayo yamewakusanya washiriki kutoka jamii za rangi, makabila na makundi mbalimbali ya Kiislamu.
Ni wazi kuwa mashindano hayo ni chuo kikuu muhimu kwa ajili ya kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.
Hayo yamesemwa na Jabir Ibrahim Mahmoud Swabir, mwanachuo kutoka nchini Sudan ambaye ameshiriki katika duru hii ya pili ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani kwa wanachuo wa Kiislamu ambayo yamemalizika hivi karibuni mjini Tehran. Amesema mashindano hayo yamekuwa mfano mzuri wa umoja unaopasa kutawala miongoni mwa Waislamu. Amesema, washiriki wa mashindano hayo wamepata fursa ya kukutana na wanazuoni muhimu wa ulimwengu wa Kiislamu na kushirikiana kwa karibu na wenzao kutoka pande mbalimbali za dunia na hivyo kuwadhihirishia walimwengu umoja unaopasa kutawala miongoni wa Waislamu na kuondoa chuki kati yao. Mahmoud amevutiwa sana na hali ya kuwa washiriki wengi wa mashindano hayo pamoja na kuwa hawawezi kuzungumza vizuri lugha ya Kiarabu lakini wanasoma Qur'ni kwa njia nzuri na ya kuvutia mno na bila ya kuvunja sheria zozote za usomaji wa kitabu hicho kitakatifu. Amesema, kushiriki katika mashindano hayo ya kimataifa kunawapa moyo wa kujiamini wasomaji wa Qur'ani na hivyo kuwawezesha kuonyesha vipawa vyao katika usomaji wa kitabu hicho bila kuogopa. Mahmoud Swabir amesema kuwa, kushirikishwa kwa wasomaji mashuhuri wa Qur'ani kama vile Sheikh Abul Ainein Sheisha na Ahmad Ahmad Nuaina kutoka Misri katika mashindano hayo ni ishara ya wazi ya namna waandaaji wa mashindano hayo wanavyoipa Qur'ani Tukufu umuhimu mkubwa. Mwishoni amewataka washindani wote walioshiriki katika mashindano hayo kuwa wajumbe halisi wa kutekeleza kivitendo mafundisho na aya walizosoma katika mashindano hayo, na sio kuwa wasomaji tu wasiotekeleza mambo wanayowasomea wenzao. 320045