IQNA

Hafla ya Usomaji wa Qur’ani Tukufu Yafanyika katika Haram ya Al-Askari nchini Iraq

11:37 - June 09, 2026
Habari ID: 3482341
IQNA – Hafla tukufu ya usomaji wa Qur’ani Tukufu iliandaliwa mwishoni mwa wiki iliyopita ndani ya Haram Takatifu ya Al-Askari iliyoko Samarra, nchini Iraq.

Maqarii kutoka Jamia ya Kisayansi ya Qur’ani Tukufu, taasisi inayofungamana na Ofisi ya Usimamizi (Astan) ya Haram ya Hadhrat Abbas (as), walishiriki katika mkusanyiko huo wa kiroho. Kwa mujibu wa ripoti ya al-Kafeel, ushiriki wa maqarii hao uliwezekana kutokana na ushirikiano madhubuti na Kituo cha Qur’ani Tukufu cha Diwaniyah kilicho chini ya jamia hiyo.

Haram ya Al-Askari, inayofahamika pia kama Msikiti wa Askariyya, ni mahala patakatifu walipolazwa Maimamu watukufu wa kumi na wa kumi na moja wa Nyumba ya Mtume (Ahlul-Bayt), yaani Al-Imam al-Hadi (as) na Al-Imam Hassan al-Askari (as).

Hafla hiyo ni mwendelezo wa juhudi za Jamia hiyo katika kuhakikisha uwepo wa kudumu kwenye harakati na programu za Qur’ani zinazofanyika katika maeneo matakatifu (Ataba) nchini Iraq.

Harakati za Qur’ani zimepata mwamko na maendeleo makubwa nchini Iraki tangu kuanguka kwa utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein mwaka 2003. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la programu za Qur’ani zikiwemo mashindano, hafla za usomaji, na kozi za mafunzo ya kielimu nchi nzima.

3497766

captcha