
Programu hiyo ya mafunzo pamoja na warsha kwa vijana Waislamu imefanyika tarehe 7 Juni 2026, kwa lengo la kuimarisha ushiriki wao wa kidini na kijamii pamoja na kuimarisha utambulisho wao wa Kiislamu ndani ya jamii ya Korea, kwa mujibu wa tovuti ya Muslimsaroundtheworld.
Katika jamii ya Waislamu nchini Korea Kusini, ambayo bado ni ndogo lakini inaendelea kukua, vijana wanachukuliwa kuwa nguzo muhimu ya mustakabali wa Uislamu nchini humo. Katika Msikiti Mkuu wa Seoul, programu za elimu na mafunzo zinazochanganya maarifa ya dini na malezi ya tabia njema, pamoja na kuimarisha hisia ya umoja na utambulisho wa Kiislamu, zinaendelea kufanyika.
KMF imesema kuwa programu hiyo imefanyika katika ukumbi wa mihadhara uliopo ghorofa ya kwanza ya jengo la nyongeza la Msikiti Mkuu wa Seoul.
Programu hiyo imelenga vijana Waislamu wa shule za kati na sekondari, na inajumuisha shughuli za kielimu, majadiliano ya duara (roundtable), pamoja na warsha zinazoshughulikia masuala yanayohusiana na elimu ya Kiislamu, mwelekeo wa taaluma, na shughuli za vijana katika siku zijazo.
Waandaaji wa programu hiyo wametangaza kuwa mbali na kutoa fursa ya mazungumzo, mawasiliano na kubadilishana uzoefu kati ya wanajamii wa Kiislamu, programu hiyo pia inalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za Kiislamu na kuimarisha hisia yao ya umoja na utambulisho wa Kiislamu.
Mkusanyiko huo umesaidia kuunda mtandao wa vijana Waislamu nchini Korea Kusini na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika programu za elimu na ulinganiaji chini ya usimamizi wa KMF.
Shirikisho la Waislamu la Korea ndilo taasisi kuu ya Kiislamu nchini Korea Kusini, likisimamia Msikiti Mkuu wa Seoul pamoja na shughuli nyingi za kidini, kielimu na ulinganiaji kote nchini.
Katika wiki za hivi karibuni, shirikisho hilo limeandaa programu mbalimbali, zikiwemo khutba za Ijumaa za kila wiki kwa lugha za Kiarabu, Kikorea na Kiingereza ili kuwahudumia Waislamu wa mataifa mbalimbali.
Taasisi hiyo pia hutoa kozi maalumu za kila mwezi kwa Waislamu wapya na wale wanaotaka kujifunza kuhusu Uislamu, pamoja na shughuli za kielimu zinazoendelea kwa vijana na watoto.
Msikiti Mkuu wa Seoul ulioko katika wilaya ya Itaewon katika mji mkuu wa Korea Kusini, umekuwa jengo maarufu zaidi la Kiislamu nchini humo tangu kufunguliwa kwake mwaka 1976, na unatumika kama kituo kikuu cha maisha ya kidini na kielimu kwa jamii ya Waislamu nchini Korea Kusini.
3497751