Hii leo suala la mazungumzo na kubadilishana mawazo kati ya mataifa na dini mbalimbali limekuwa maudhui muhimu, na mikutano na makongamano mengi ya kieneo, kitaifa na kimataifa yamekuwa yakifanyika katika uwanja huo. Maudhui hiyo aidha imepewa nafasi muhimu na makhsusi katika utamaduni wa Kiislamu. Dini hii daima huwahimiza wafuasi wake kutumia njia ya mazungumzo, uvumilivu na subira katika kuhubiri mafundisho yake kwa watu wengine. Qur'ani, kikiwa ni kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu, imelizingatia sana la kulichunguza suala la mazungumzo na kubadilishana mawazo katika pande kadhaa. Mfano wa kwanza kabisa wa mazungumzo ya Qur'ani Tukufu ni yale yaliyofanyika kati ya Mwenyezi Mungu na Malaika kuhusiana na Nabii Adam A.S, pale alipowakusanya Malaika wake na kuwapasha habari ya kutaka kuumba mwanadamu na kumpa madaraka katika ardhi kama inavyosema aya ya 30 ya Suratul Baqarah ambapo Malaika nao pia walianza mazungumzo na Mola wao Mlezi na kutoa maoni yao juu ya kiumbe huyo mpya anayetaka kuumba. Aya hiyo inasema:
وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلاَئِكَةِ إِنِّی جَاعِلٌ فِی الأَرْضِ خَلِيفَةً قَالُواْ أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن یُفْسِدُ فِيهَا وَیَسْفِكُ الدِّمَاء وَنَحْنُ نُسَبِّحُ بِحَمْدِكَ وَنُقَدِّسُ لَكَ قَالَ إِنِّی أَعْلَمُ مَا لاَ تَعْلَمُونَ
(Wakumbushe watu habari hii) wakati Mola wako Mlezi alipowaambia Malaika: Mimi nitaweka viumbe wengine katika ardhi. Malaika wakasema: utaweka humo watakaofanya uharibifu na kumwaga damu hali sisi tunakutukuza kwa sifa zao na kukutaja kwa utakatifu wako? Mwenyezi Mungu akasema: Hakika mimi nayajua msiyoyajua". Aya za kitabu hicho kitukufu pia zimenukuu mazungumzo mengi yaliyofanyika kati ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake na kati ya Mitume na umma zao kwa nia ya kutaka kuwaongoa na kuwaelekeza katika njia iliyonyooka. Si hayo tu bali Qur'ani imetunukulia mijadala na mazungumzo yaliyofanyika baina ya binadamu na wanyama kama yale yaliyofanyika kati ya Nabii Sulaiman na ndege “Hud-hud” aliyekuwa chini ya utawala na mamlaka yake. Aya ya 22 ya Suratun Naml inatunukulia mazungumzo ya ndege Hud-hud akimuhutubu Nabii Sulaiman kwa kusema:
فَمَكَثَ غَیْرَ بَعِيدٍ فَقَالَ أَحَطتُ بِمَا لَمْ تُحِطْ بِهِ وَجِئْتُكَ مِن سَبَإٍ بِنَبَإٍ یَقِينٍ
Basi hakukaa sana, mara Hud-hud akafika na kumwambia Nabii Sulaiman: Nimegundua usilogundua na ninakujia hivi sasa kutoka nchi inayoitwa Sabaa na kukuletea habari yenye yakini.…” Aya ya 27 ya sura hiyo hiyo inatunukulia majibu ya Nabii Sulaiman kwa ndege huyo akisema: قَالَ سَنَنظُرُ أَصَدَقْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْكَاذِبِينَ
Tutatazama kama umesema kweli au umo katika warongo".
Katika mtazamo wa Qur'ani, mazungumzo kati ya wanadamu hayapaswi kufanyika bila ya malengo yoyote na wala katika njia ya batili. Mazungumzo kati ya pande mbili au pande kadhaa yanapaswa kuwa na mwelekeo na malengo maalumu ili yaweze kuzaa matunda. Miongoni mwa malengo ya kuwepo mazungumzo kama hayo ni kukomesha uhasama na uadui kati ya pande hasimu zinazotofautiana. Katika uwanja huo Qur’ani inawaamuru Waislamu kutumia njia bora za mijadala na mazungumzo katika kukomesha uhasama na mijadala ya kiitikadi na kidini. Aya ya 34 ya Suratu Fusswilat inasema: ادْفَعْ بِالَّتِی هِیَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِی بَیْنَكَ وَبَیْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِیٌّ حَمِيمٌ
“Lijibu jambo baya kwa tendo jema, ili yule ulioko uadui baina yako na yeye abadilike na kuwa rafiki yako wa karibu.” Hii ina maana kwamba, Mwenyezi Mungu anawataka Waislamu kutumia njia ya mazungumzo katika kutatua hitilafu zilizopo kwa kadiri ya kumfanya hata adui sugu kuwa rafiki wa karibu au wa “chanda na pete” kama wasemavyo Waswahili.
Mbali na kuwataka Waislamu kutumia njia ya mazungumzo kuondoa uhasama na uadui, Uislamu pia unawataka wanadamu kutumia njia ya kubadilishana mawazo na mazungumzo kujenga umoja na mshikamano kati ya kaumu, mataifa na makundi mbalimbali. Aya ya 64 ya Suratu Ali Imran inaweka wazi uhakika huo. Aya hiyo inasema:
قُلْ یَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْاْ إِلَى كَلَمَةٍ سَوَاء بَیْنَنَا وَبَیْنَكُمْ أَلاَّ نَعْبُدَ إِلاَّ اللّهَ وَلاَ نُشْرِكَ بِهِ شَیْئًا وَلاَ یَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضاً أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللّهِ
Sema: Enyi watu mlioteremshiwa kitabu cha Mwenyezi Mingu (Mayahudi na Manasara), njooni kwenye neno lililosawa baina yetu na ninyi ya kwamba, tusimwabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu mmoja na wala tusimshirikishe na chochote, na wala tusiwafanye baadhi yetu kuwa miola ya wengine badala ya Mwenyezi Mungu…". Mtume Muhammad SAW pia alitumia aya hii katika barua alizowatumia wafalme wa tawala mbalimbali za wakati huo akiwalingania kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja.
Qur’ani Tukufu pia imeyatambua mazungumzo na kutoa dalili na hoja kuwa ndiyo njia bora zaidi ya kulingania na kuwaongoza wanadamu, kwani mafundisho ya Uislamu kwa mtazamo huo ndiyo haki na kweli, na kila mtu mwenye insafu na mkweli hukubali hoja hizo. Aya za 17 na 18 za Suratuz Zumar zinasema:
فَبَشِّرْ عِبَادِ * الَّذِينَ یَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَیَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ أُوْلَئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّهُ وَأُوْلَئِكَ هُمْ أُوْلُوا الْأَلْبَابِ
"Wape bishara njema waja wangu, ambao husikiliza kauli (nyingi zinazosemwa) wakafuata zilizobora zaidi. Hao ndio walioongozwa na Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili”.
Kwa msingi huo, katika mtazamo wa Qur’ani mazungumzo na kubadilishana mawazo ni jambo la dharura na lenye athari na faida kubwa.
Pamoja na hayo, ili mazungumzo na mijadala ya kubadilisha fikra na mawazo iwe na faida hapana budi kuwepo masharti kadhaa. Miongoni mwa masharti hayo ni yale yaliyotajwa kwenye aya ya 64 ya Suratu Aali Imran kama vile kuwepo itikadi ya Mwenyezi Mungu mmoja kati ya pande mbili zinazozungumza na kujadiliana na kutomshirikisha na chochote. Katika Qur’ani Tukufu pia kuna aya zinazomuamuru Mtume Mtukufu kuwapa hifadhi washirikina wenye hamu ya kusikiliza neno la Mungu, na kumkataza kufanya mazungumzo na wapinzani makaidi na wenye taasubi na chuki za kidini, kwa kuzingatia ukweli kwamba, watu wa aina hii hawako tayari kukubali haki na hoja za wazi, na kwa hivyo ni upuuzi na hatua isiyokuwa na matunda kujadiliana na kuzungumza na watu kama hao. Aya ya sita ya Suratut Tauba inasema: وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّى یَسْمَعَ كَلاَمَ اللّهِ
“Na iwapo mmoja kati ya Washirikina atakuomba hifadhi basi mpe hifadhi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu…”
Miongoni mwa masharti na mjadala wa kubadilishana mawazo na mazungumzo ni kila upande kuukubali na kuutambua mwingine. Hata hivyo tunapaswa kuashiria hapa kuwa, kukubali upande wa pili wa mazungumzo hakuna maana ya kukubaliana na fikra na mitazamo yake ya kiitikadi. Qur’ani Tukufu inalitaja sharti jingine la mazungumzo yenye mafanikio kuwa ni elimu na ujuzi wa pande mbili zinazozungumza kuhusu maudhui inayojadiliwa. Kimsingi katika dini ya Kiislamu elimu na ujuzi huzingatiwa kuwa ni fadhila na sifa aali na bora , na iwapo pande mbili zinazozungumza zitakosa sifa ya kuwa na maarifa na elimu ya kutosha juu ya kile kinachojadiliwa, bila shaka mjadala na mazungumzo hayo hayatafikia hatima ya kuridhisha, bali yumkini yakakosa mwelekeo na kupoteza njia yake. Kwa sababu hiyo katika aya ya 36 ya Suratul Israa, Mwenyezi Mungu anamtaka mwanadamu kutofuata kile asichokuwa na ilimu nacho. Aya hiyo inasema:
وَلاَ تَقْفُ مَا لَیْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولـئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْؤُولاً
"Wala usifuate usiyokuwa na elimu nayo, hakika masikio, macho na moyo vyote vitaulizwa".
Kulinda misingi ya adabu na heshima ni jambo muhimu na linalopaswa kupewa kipaumbele katika aina yoyote ya mijadala ya kubadilishana mawazo na mazungumzo ya pande mbili. Qur'ani inataja moja ya misingi hiyo kuwa ni kuheshimu fikra na matukufu ya upande wa pili. Aya nyingi za kitabu hicho zinawakemea na kuwalaumu wale wanaowafanyia stihizai na kuwakejeli Mitume wa Mwenyezi Mungu. Aya ya 108 ya Suratul An-am inawaambia Waislamu kwamba:
وَلاَ تَسُبُّواْ الَّذِينَ یَدْعُونَ مِن دُونِ اللّهِ فَیَسُبُّواْ اللّهَ عَدْوًا بِغَیْرِ عِلْمٍ
"Wala msiwatukane wale wanaomuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu mmoja wasije nao wakamtusi Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua…". Katika upande mwingine Uislamu unazitaka pande mbili zinazozungumza kutopandisha juu sauti wakati wa mazungumzo na kujadiliana kwa opole na kwa kutumia hoja za kimantiki na za wazi bila ya kuingia kwenye malumbano. Qur’ani Tukufu yenyewe imetumia mbinu hiyo hiyo na Mtume Muhammad SAW aliheshimu misingi hiyo wakati wa kuwalingania watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Aya ya 125 ya Suratun Nahl inasema:
ادْعُ إِلِى سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِی هِیَ أَحْسَنُ
"Lingania watu njia ya Mola wako Mlezi kwa kutumia hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa namna iliyo bora".
Kuhusiana na namna ya kufanya mazungumzo pia Mwenyezi Mungu anawakataza Waislamu kuzungumza kwa sauti kubwa na ya juu na kuwalazimisha watu kukubali haki na ukweli. Siri ya mafanikio ya Mtume wa Mwenyezi Mungu katika kuwavutia watu kwa mtazamo wa Qur'ani, ni akhlaki, mwenendo wake mwema, na kuzungumza kwa upole na kutumia maneno laini na watu. Aya za 43 na 44 za Suratu Twaha zinawaamuru Manabii Musa na Harun kuzungumza kwa upole na kwa maneno laini na watu waasi na waliokengeuka mipaka kama vile Firauni, asaa wakaongoka kwa kuwaidhika na maneno yao au kwa kuogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Wakati mazungumzo kati ya pande mbili yanapofanyika kwa msingi wa hoja na mantiki basi hapana haja ya kutwishana itikadi na mitazamo ya upande mmoja juu ya mwingine, na hatimaye kila upande huweza kujichagulia njia ya haki na kweli kwa uhuru kamili. Qur'ani inasisitiza kuwa, si sahihi kuwalazimisha watu kuukubali Uislamu, kama inavyosema aya ya 256 ya Suratul Baqarah kwamba:
لاَ إِكْرَاهَ فِی الدِّينِ قَد تَّبَیَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَیِّ
"Hakuna kulazimishana katika dini, kwani njia ya uongofu na haki imebainika wazi na kujitenga na opotofu".
Hata hivyo hapana budi kuashiria nukta hii kwamba, aya za Qur'ani Tukufu zinazozungumzia haja ya kuwepo mazungumzo zimeweka wazi pia kwamba, mazungumzo si njia ya kutumiwa daima dawamu na katika kila mazingira. Kwa mfano wakati madola ya kibeberu yanapoyachokoza na kuyavamia mataifa mengine kwa nia ya kupora utajiri na mali zao, hapa Qur’ani inawaamuru watu wa mataifa hayo yanayodhulumiwa kujihami na kujizatiti kwa hali na mali kwa ajili ya mapambano na kutetea haki zao. Katika hali kama hii haipaswi kuingia kwenye mijadala na mazungumzo yasiyokuwa na faida yoyote, kwani mazungumzo kama hayo humpa adui fursa ya kujiimarisha zaidi na kuwatokomeza kwa urahisi wale waliochini ya dhulma na uonevu.
Ni matumaini yetu kuona pande zote zinazozozana na kuhitilafiana zikitumia njia ya mazungumzo ya kimantiki na hoja za wazi -kama inavyobainisha Qur'an- katika kutatua hitilafu zao.