Ataullah Hanna, Mkuu wa Kanisa la Orthdox katika mji mtakatifu wa Quds ametoa matamshi ya kuzikosoa nchi za Magharibi kwa kusema kuwa, kuzingirwa Ukanda wa Gaza ni natija ya juhudi za nchi hizo za eti kuleta amani katika Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa tovuti ya Quds Online, Hanna amebainisha hali ya kusikitisha ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, kuungwa mkono wakazi Wa Ukanda huo wanaoteseka chini ya mzingiro wa kidhulma unaotekelezwa dhidi yao na utawala haramu wa Israel, ni wadhifa na jukumu la kibinadamu na kimaanawi la kila mtu. Amesema, mivutano inayoonekana kati ya makundi mbalimbali ya Kipalestina imeathiri vibaya umoja wa Wapalestina na kufanya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ziendelee kudhibitiwa. Ataullah Hanna ameendelea kusema kuwa, Wapalestina wanaweza tu kuishi katika mazingira ya uhuru na kujitawala, kulinda utukufu wao na hatimaye kukomboa ardhi zao kutoka kwenye makucha ya maghasibu wa Israel, kwa kulinda umoja na mshikamano wao. Amesema, Wakristo wa Palestina daima wamekuwa wakilinda utambulisho wao wa Kiarabu na kwamba ni miongoni mwa watetezi wa mwanzo kabisa wa ardhi za Wapalestina ambazo hivi sasa zinakaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel. 332993