IQNA

Katibu Mkuu wa Isesco ataka kuzingatiwa mazungumzo ya staarabu

12:14 - April 08, 2009
Habari ID: 1761947
Abdul Aziz Othman al-Tuwaijri, Katibu Mkuu wa Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ISESCO, amewataka watu kuzingatia zaidi masuala ya kueneza utamaduni wa amani, kuishi pamoja kwa amani wanadamu na kuheshimiwa sheria za kimataifa pamoja na hati ya haki za binadamu kote ulimwenguni.
Akizungumza katika kikao cha pili cha Muungano wa Staarabu huko nchini Uturuki, al Tuwaijri amesema kuwa kuzingatiwa mawasiliano ya kimaanawi na Mwenyezi Mungu pamoja na mafundisho ya kidini ni moja ya njia zinazomuelekeza mwanadamu katika ustawi na maendeleo. Amesema kwamba iwapo viongozi na watawala hawatazingatia na kuchukua hatua za lazima kwa madhumuni ya kuimarisha amani na utulivu duniani, ni wazi kwamba jamii ya mwanadamu itaangamia.
Katibu Mkuu wa Isesco amesema, ulimwengu hii leo unahitaji kuwa na uhusiano wa kiutamaduni na kijamii kuliko wakati mwingine wowote ule na kwa hivyo tunapasa kuimarisha suala hilo kupitia mazungumzo, kama tunavyofanya katika kuimarisha uhusiano wetu wa kisiasa. Al-Tuwaijri amesema kuwa inashangaza kuona kwamba katika hali ambayo watu wengi ulimwenguni wanatoa nara za kuwepo amani na utulivu duniani, lakini hakuna juhudi zozote za maana zinazochukuliwa kuhusiana na suala hilo bali baadhi ya madola hufanya juhudi za makusudi za kuvuruga amani na usalama ulimwenguni na kukunyaga bila kujali, sheria za kimataifa pamoja na maazimio ya Umoja wa Mataifa kwa madhara ya jamii ya mwanadamu.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba, licha ya kuwa miaka 64 imepita sasa tokea kuasisiwa Umoja wa Mataifa na 61 tokea kupitishwa Azimio la Haki za Binadamu, lakini kwa masikitiko makubwa bado kuna madola makubwa duniani yanayotekeleza siasa za kimaslahi na kikoloni kwa madhara ya jamii ya mwanadmu.
al Tuwaijri ameashiria mgogoro wa fedha wa hivi sasa duniani na kusema kuwa unatokana na tamaa ya baadhi ya madola na watu wanaotaka kujitajirisha kwa kila njia, watu ambao wanapambana dhidi ya mazungumzo ya staarabu mbalimbali kwa sababu wanayachukulia mazungumzo hayo kuwa hatari kubwa kwa maslahi yao haramu. 384296
captcha