IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu yalaaniwa katika kikao cha Baraza la Kiislamu la Eurasia

12:56 - May 17, 2009
Habari ID: 1779320
Kikao cha saba cha Baraza la Kiislamu la Eurasia kilimazika siku ya Ijumaa kwa kutolewa taarifa ya kulaani siasa za kichochezi na chuki dhidi ya mafundisho ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa gazeti la Today Zaman, washiriki wa kikao hicho walitoa taarifa ya pamoja wakisema kuwa kuenezwa chuki dhidi ya Uislamu ni sawa kabisa na ugaidi na wakati huohuo kulaani jambo hilo. Wamesema kuwa kuenezwa chuki na woga dhidi ya Uislamu ni kizuizi kikubwa katika juhudi za kuimarisha amani na uthabiti ulimwenguni. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa, maisha katika kivuli cha amani na heshima ya pande mbili ni jambo la kimsingi katika mafundisho ya Uislamu na moja ya mahitaji muhimu ya mwanadamu. Moja ya maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao hicho ni kufanyika juhudi za ziada kwa lengo la kutarjumiwa kwa lugha mbalimbali vitabu vya wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu barani Ulaya na Asia ili watu wapate fursa ya kunufaika navyo. Kuwasilishwa kwa njia za kuzuia kufanyika makosa katika tarjumi ya Qur'ani katika lugha nyinginezo na kuchunguzwa tofauti za tarehe katika nchi za Kiislamu ni mambo mengine yaliyopewa uzito katika kikao hicho. Kikao hicho ambacho kilifanyika siku ya Jumanne tarehe 12 Mei katika Hoteli ya Intercontinental huko mjini Istanbul Uturuki, kilihudhuriwa na wanazuoni na wasomi zaidi ya 100 kutoka nchi 42 za Ulaya na Asia. 405676
captcha