Kamati hiyo itakayowajumuisha wataalamu wa Ulaya, itapitia upya vitabu vinavyotumiwa na nchi za Magharibi kutoa mafunzo kuhusu Uislamu na kufuta vipengee vinavyotoa picha mbaya na isiyokuwa sahihi kuhusu dini hiyo.
Uamuzi huo umechukuliwa baada ya kushadidi wimbi la mashambulizi ya propaganda chafu dhidi ya dini Kiislamu kupitia vitabu vinavyotumiwa kufundisha mashuleni barani Ulaya.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Geneva Fauzia Ashmawi amesema kuwa vitabu vya masomo katika shule na vyuo vikuu vya Ulaya vina mambo yasiyokuwa sahihi na ya kupotosha kuhusu Uislamu na Waislamu, Mtume Muhammad na mitazamo ya Uislamu kuhusu mwanamke.
Ashmawi amesema kuwa mtazamo wa Magharibi kuhusu Uislamu umejengeka juu ya ujahili na uzushi na kwamba baadhi ya watu wenye misimamo mikali huko Magharibi wanaeneza fikra za uongo kwamba dini ya Kiislamu ilienea kwa kutumia upanga.
Mhadhiri huyo wa chuo kikuu amesema Vitabu vingi vya kufunzia Uislamu vinavyotumiwa katika shule za Ufaransa, Ujerumani, Austria, Uswisi na Denmark vina masuala ya uzushi na yasiyokuwa sahihi kuhusu Mtume Muhammad (saw) sheria za Uislamu na Waislamu wenyewe. 429415