IQNA

Idara ya Haramu Takatifu ya Hadhrat Abbas (AS) yakamilisha urekebishaji wa Msahafu adimu

15:20 - June 07, 2026
Habari ID: 3482331
IQNA – Idara ya Masuala ya Kifikra na Utamaduni ya Astan au Mamlaka ya Usimamizi ya Haramu Takatifu ya Hadhrat Abbas (AS) iliyopo Karbala, Iraq, imekamilisha kazi kubwa ya urekebishaji wa nakala adimu na yenye thamani ya kipekee ya Qur’ani Tukufu.

Kituo cha Al-Fadl cha Uhifadhi wa Urithi wa Maandishi ya Kale na Nyaraka kilichopo chini ya Maktaba ya Astan, kimesimamia na kutekeleza urekebishaji huo kwa kufuata viwango vya juu zaidi vya kisayansi na kiufundi vinavyotumiwa kimataifa katika uhifadhi wa maandishi ya kale (manuscripts).

Bwana Laith Lutfi, ambaye ni Mkurugenzi wa kituo hicho, amebainisha kuwa wataalamu wa kituo hicho wamekamilisha ukarabati wa nakala hiyo, ambayo inatajwa kuwa miongoni mwa maandishi adimu zaidi yanayohifadhiwa katika Hazina ya Haramu ya Kadhimiya.

Aliongeza kuwa mchakato huo wa ukarabati ulipita katika hatua kadhaa za kitaalamu, ikiwa ni pamoja na kuifanyia nakala hiyo kumbukumbu ya picha na maandishi, kupanga kurasa zake kwa kufuata mlolongo wa nambari, pamoja na kufanya vipimo muhimu vya kibaolojia na kikemia ili kubaini hali yake na kuweka mbinu sahihi za uhifadhi.

Lutfi alifafanua kuwa timu hiyo ya wataalamu ilitekeleza mfululizo wa hatua makini za kiufundi, ikiwemo usafishaji wa kimitambo (mechanical cleaning), kubadilisha sehemu zilizopotea au kuharibika, ushonaji na ujalidi (binding), pamoja na mbinu nyingine za kitaalamu zilizosaidia kuirejesha nakala hiyo katika hali yake bora na kulinda thamani yake ya kielimu na kiurithi.

Alisisitiza kuwa ukarabati huo unasaidia kurefusha maisha ya maandishi hayo adimu, kuikinga na uharibifu, na kuhakikisha kuwa thamani yake ya kihistoria na kielimu inafika kwa vizazi vijavyo kwa usalama.

Wakati huo huo, kituo hicho kinaendeleza juhudi zake za kuhifadhi na kukarabati maandishi na nyaraka adimu, kikilenga kulinda na kurithisha urithi mtukufu wa Kiislamu kwa vizazi vijavyo.

3497743

Habari zinazohusiana
captcha