IQNA

Polisi wa London wafahamishwa mafundisho ya Kiislamu

23:21 - September 19, 2010
Habari ID: 1997031
Baadhi ya polisi wa London nchini Uingereza siku ya Ijumaa walishiriki katika mafundisho ya Waislamu na kufahamishwa baadhi ya mafunzo ya dini tukufu ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa Stargazete Polisi hao ambao walihudhuria vikao vya mafundisho ya Kiislamu katika msikiti wa Maulana ambao ni wa Waturuki wanaoishi mjini London, walionana na kuzungumza kwa karibu na Waislamu pamoja na wanazuoni wa Kiislamu katika msikiti huo. Fatih Kahraman ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa msikiti huo alitoa maelezo muhimu kuhusiana na falsafa ya swala, ujenzi wa misikiti na maana ya maandishi, michoro na nembo za Kiislamu zinazotumika katika maeneo ya ibada.
Katika sehemu nyingine ya mazungumzo hayo ya kiutamaduni, polisi hao wa London waliuliza maswali kadhaa yanayohusiana na sheria za Kiislamu na kupewa majibu ya kuridhisha na wanazuoni wa Kiislamu waliokuwa msikitini hupo.
Vilevile polisi hao waliashiria tukio la kusikitisha la kuchomwa moto Qur'ani nchini Marekani na kulaani vikali tukio hilo ambalo wamesema linaweza kuzusha mivutano na mifarakano miongoni mwa wananchi. Polisi hao pia wamesisitiza juu ya kulindwa umoja na mshikamano wa wananchi wa Uingereza na kuimarishwa mazungumzo kati yao. 657277
captcha