Kikao cha cha nne cha Muungano wa Idhaa na Televisheni za Kiislamu kilimalizika jana Jumanne mjini Tehran kwa hotuba iliyotolewa na Izzatullah Dharghami, Mkuu wa Taasisi ya Redio na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Soko la pili la filamu za Kiislamu na vilevile tamasha la pili la uzalishaji vipindi vya wanachama wa muungano huo pia lilifanyika mwishoni mwa kikao hicho ambapo washindi wa vipindi bora walitunukiwa zawadi na loho za kushukuru juhudi zao katika uwanja wa upashaji habari na uzalishaji filamu.
Akizungumzia suala la kupigwa marufuku filamu ya Basharat Munji iliyotengenezwa na Nader Talibzadeh ambaye pia alihudhuria sherehe za kumalizika kikao hicho, Muhandisi Dharghami amesema kuwa marufuku hiyo ni kama kuitangaza filamu hiyo duniani kwa sababu haki haiwezi kufunikwa wala kubanwa, na kwamba hatimaye itapenya na kutafuta njia ya kuwafikia walimwengu.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita ambapo harakati kubwa imekuwa ikifanywa na maadui kwa lengo la kuzuia kuenea Uislamu duniani, ukiwemo uchomaji moto na kukosewa heshima Qur'ani Tukufu, jambo hilo limekuwa na matokeo kinyume na walivyotarajia maadui, na hata kusaidia kufahamika zaidi dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu duniani. 673950