Kufuatia upinzani wa Waislamu wa jimbo la Oklahoma dhidi ya kupigwa marufuku utumiwaji wa sheria za Kiislamu katika mahakama za jimbo hilo, Waislamu hao wamepeleka malalamiko yao katika Mahakama Kuu ya Marekani ili kuchunguzwa na kushughulikiwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Times, Munir Awad, mkuu wa Baraza la Uhusiano wa Kiislamu na Marekani tawi la Oklahoma amesema kuwa Waislamu wamelazimika kufikisha malalamiko yao katika Mahakama Kuu baada ya kuchukuliwa uamuzi wa kupinga kutumiwa sheria za Kiislamu katika mahakama za jimbo la Oklohama.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo, Awad anaamini kuwa matokeo ya kura ya maoni katika jimbo hilo yaliyopelekea kupigwa marufuku utumiwaji wa sheria za Kiislamu ni ya ubaguzi wa kidini ambayo hayapaswi kuzingatiwa. Amesema kuwa jambo hilo limelenga kupinga Uislamu katika jimbo hilo. Awad amesema kuwa masuala yanayohusiana na sheria za Kiislamu zikiwemo za urithi, ndoa na talaka zinapaswa kuachiwa wataalamu wa masuala ya Kiislamu na sio mahakimu wasiojua lolote kuhusiana na sheria hizo.
Kwa kuongezeka kwa kasi idadi ya Waislamu wanaoishi katika nchi za Ulaya na Marekani katika miaka ya hivi karibuni, umuhimu wa kutumika sheria za Kiislamu katika mahakama za kisekula za nchi hizo umeongezeka maradufu. 699977