Kongamano hilo limesimamiwa na Kituo cha Utafiti wa Hauza cha al Huda cha Najaf kikishirikiana na Kituo cha Utafiti cha Iraq na Jumuiya ya Wahadhiri wa chuo hicho. Kongamano hilo limehudhuriwa na wahadhiri wa vyuo vikuu, walimu wa vyuo vya kidini, shakhsia na wanasiasa wa Iraq.
Washiriki katika kongamano hilo wamechunguza na kuzungumzia mchango wa Imam Khomeini na Ayatullahil Udhma Shahid Muhammad Baqir Sadr katika medani za siasa na elimu na taathira za shakhsia hao wawili wa Kishia katika mafanikio ya harakati ya mabadiliko katika ulimwengu wa Kiislamu.
Khalid Abdul Wahhab al Mulla ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maulamaa wa Ahlul Sunna ya Iraq amehutubia kongamano hilo akisema kuwa Imam Khomeini na Shahid Baqir al Sadr wamewafundisha Waislamu wa zama hizi jinsi ya kuwa na misimamo ya wastani na kulingania umoja na mshikamano wa Kiislamu.
Imam wa swala ya Ijuma ya mji mtakatifu wa Najaf Sayyid Sadruddin al Qubanchi pia amehutubia kongamano hilo akisema kuwa wanazuoni hao wawili wakubwa walikuwa vinara wa harakati ya mwamko wa Kiislamu. 702681