IQNA

Zaidi ya Watu 60 wauawa katika maombolezo ya Ashura, Afghanistan

15:55 - December 07, 2011
Habari ID: 2234738
Waombolezaji zaidi ya 60 wa Imam Hussein bin Ali (as) wameua shahidi kufuatia mashambulio yaliyotekelezwa jana na magaidi katika siku ya Ashura katika miji tofauti ya Afghanistan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters makumi ya waombolezaji waliuawa katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa na magaidi mjini Kabul, mji mkuu wa Afghanistan na wengine kadhaa kuuawa katika mji wa Mazar Shariff.
Mashambulio hayo dhidi ya waombolezaji wa Imam Hussein (as) yalikuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tokea wakati wa kuanguka utawala wa Taliban.
Rais Hamid Karzai ambaye alikuwa na lengo la kusafiri katika nchi kadhaa za Ulaya baada ya kumalizika kikao cha kimataifa cha mustakbali wa Afghanistan huko Bonn Ujerumani, alikatiza safari yake hiyo na kurejea nchini kwake ili kufuatilia na kuchunguza matukio hayo kwa karibu.
Akizungumza mbele ya waandishi bahari mara tu baada ya kurejea nchini, Rais Karzai alisema kuwa hilo ndilo shambulio kubwa zaidi la kigaidi kuwahi kufanyika dhidi ya waombolezaji wa kidini nchini humo katika siku muhimu kama hii. Karzai ameongeza kuwa maadui wa Afghanistan wanataka kuleta mifarakano ya kimadhehebu nchini kupitia mashambulio hayo ya kigaidi.
Katika upande wa pili, wanazuoni wa Kishia wa Afghanistan wametoa taarifa wakilaani vitendo hivyo vya kigaidi dhidi ya Mashia na kuomboleza na familia za mashahidi wa matukio hayo ya kusikitisha. Wamewataka waombolezaji kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu na kushirikiana na maafisa usalama ili kuwatia nguvuni wahusika wa ugaidi huo dhidi ya watu wasio na hatia. 911393
captcha