Harakati ya Amal Islamu ya Lebanon imetoa taarifa ikilaani vikali mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.
Taarifa hiyo imeutaka Umoja wa Mataifa la Baraza lake la Usalama na jumuiya nyingine za kimataifa kuchukua hatua za dharura za kusimamisha mashambulizi hayo.
Wapalestina wengine wawili wameuawa shahidi hii leo na ndege za jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel na kupelekea idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi tangu kuanza duru mpya ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza kufikia 23.
Duru za hospitali za Palestina zimeripoti kuwa mashambulizi hayo yamefanywa alasiri ya leo na ndege ya kivita ya Israel dhidi ya kaskazini mwa Gaza.
Wakati hayo yakiripotiwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imekosoa utendaji dhaifu na usio na mlingano wa kanali ya Televisheni ya al Jazeera ya Qatar katika kuakisi mashambulizi ya ndege za jeshi la Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza. Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema kuwa harakati hiyo inasikitishwa na hatua ya kanali hiyo ya kutoyapa umuhimu mashambulizi hayo dhidi ya Gaza na kuashiria tu kwa ufupi suala hilo mwishoni mwa matangazo yake. 970717