IQNA

Utawala wa Kizayuni una wahaka mkubwa kuhusu uchaguzi Misri

10:03 - May 15, 2012
Habari ID: 2325918
Huku ikiwa imesalia chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi wa rais kufanyika nchini Misri, utawala wa Kizayuni umeingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu matukio ya Misri.
Kile ambacho kimezidisha wahaka na masaibu ya utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuwa wagombea wote wa urais Misri wametangaza bayana kuwa wanapinga ule Mkataba wa 'Amani' wa Camp David, limeandika gazeti la Al Akhbar la Lebanon.
Ujenzi wa ukuta wa kilomita 75 katika mpaka wa Misri na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel ni mfano wa namna uhusiano wa Cairo na Tel Aviv unazidi kudorora.
Mwezi jana Misri ilisitisha uuzaji gesi kwa utawala haramu wa Israel na kubatilisha mkataba baina ya pande mbili kuhusu uuzaji gesi jambo ambalo liliwashangaza sana wakuu wa utawala wa Kizayuni.
Ikumbukwe kuwa wagombea wakuu wa uchaguzi wa Rais nchini Misri wameiponda vikali Israel katika mdahalo wao walioufanya kupitia televisheni na kusema kuwa utawala wa Kizayuni ni adui wa taifa la Misri.
Abdel Mon'im Aboul Fotouh, kiongozi wa zamani wa harakati ya Ikhwanul Muslimin amesema, Israel ni adui, na ni utawala ambao uliasisiwa ili kukalia kwa mabavu ardhi za mataifa mengine na kuhatarisha usalama wa eneo zima la Mashariki ya Kati.
Ameongeza kuwa, Israel kwa kuwa na vichwa 200 vya nyuklia, inatishia usalama wa eneo hili zima, na licha ya hivyo bado inapinga maazimio ya kimataifa na kukwamisha juhudi za kurejeshewa Wapalestina, haki zao.
Naye Amru Musa, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Misri aliyewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, ameelezea msimamo unaofanana na huo na kuongeza kwamba wananchi wengi wa Misri wanatambua kuwa Israel ni adui yao na hawayaafiki makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya Misri na utawala huo.
Wagombea hao wawili ni miongoni mwa wengine 13 wanaogombea nafasi ya urais wa Misri katika uchaguzi utakaoanza tarehe 23 mwezi huu wa Mei.
1007439
captcha